Saturday, 8 November 2014
GHARAMA ZA MATIBABU SASA KUDHIBITIWA
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imeiagiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kupitia upya mpango wao wa kuongeza gharama za matibabu, vipimo na chakula na kisha kuuwasilisha wizarani hapo kwa ajili ya mashauriano kuepuka kuwaumiza wananchi.
Aidha wizara hiyo, imesema inaanda mwongozo wa kusimamia upandishaji wa gharama za matibabu, vipimo na chakula kwa hospitali zote nchini, zikiwemo hospitali binafsi ili kuzuia upandishwaji holela wa gharama hizo.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Donan Mbando wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam, katika hafla ya kuapisha baadhi ya makatibu wakuu, makatibu tawala, mabalozi na wakuu wa mikoa walioteuliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete.
“Tumeamua kuwaagiza wapitie kwanza mpango wao huo na kuleta kwetu mapendekezo yao ya kupandisha gharama za matibabu ili tuweze kushauriana namna ya kulishughulikia suala hili kwa kuwa kupandisha holela gharama hizi kunaumiza Watanzania,” alisisitiza Mbando.
Alisema kutokana na sababu hiyo, wizara hiyo inaandaa mwongozo ambao si tu utasimamia hospitali za Serikali katika suala zima la gharama bali utasimamia na hospitali binafsi, lengo likiwa ni kuwapunguzia mzigo wa gharama za matibabu wananchi.
Aidha Mbando alisema wizara hiyo pia katika kuhakikisha tatizo la upungufu wa dawa katika hospitali linakuwa historia, imeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali katika bajeti ijayo ya mwaka 2015/2016 iiongezee fedha za kutosha Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Alisema MSD imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya usafirishaji wa dawa hali ambayo imeifanya bohari hiyo kuzidiwa na hivyo kusababisha Serikali kuamua kuanzisha bohari ndogo katika kila mkoa na hadi sasa bohari tano zimeshaanzishwa nchi nzima.
“Lakini pia tupo katika hatua ya kati ya kuandaa mwongozo wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata bima ya afya. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kunipatia fursa hii, nitashirikiana na wenzangu kuhakikisha tunakabiliana na changamoto katika sekta ya afya,” alisema.
Mbando kabla ya uteuzi huo wa ukatibu mkuu, alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali, pamoja naye pia aliapishwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mbogo Futakamba na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifungo na Uvuvi, Dk Yohana Budeba.
Dk Budeba kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Futakamba alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji.
Wengine walioapishwa katika hafla hiyo ni Jack Zoka aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada na Samuel Shelukindo aliyeteuliwa kuwa Mshauri wa Rais Masuala ya Kidiplomasia mwenye hadhi ya Ubalozi.
Aidha Rais Kikwete katika hafla hiyo, aliwaapisha wakuu wa mikoa wapya aliowateua baada ya kuwapandisha vyeo kutoka nafasi ya ukuu wa wilaya ambao ni Halima Dendego anayekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk Ibrahim Msengi (Katavi), Amina Masenza (Iringa) na John Mongella (Kagera).
Kabla ya uteuzi huo, Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Dendego alikuwa Tanga, Masenza alikuwa Ilemela na Msengi alikuwa Moshi.
Pia aliwaapisha makatibu tawala wa mikoa wawili ambao ni Charles Pallangyo anayekwenda mkoa wa Geita na Adoh Mapunda anayekwenda Arusha.
Pallangyo kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakati Mapunda alikuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Bukoba.
Kwa upande wake Dendego, alisema anashukuru kuwa kwa sasa mkoa wa Mtwara vurugu za gesi na mafuta zimetulia na hivyo kipaumbele chake kitakuwa kuwahakikishia maendeleo na maisha bora wakazi wa mkoa huo.
Naye Futakamba alisema kwa kuwa tayari ni mzoefu na Wizara ya Maji, atahakikisha anaendeleza miradi na mikakati ya maji iliyopo ikiwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa mtambo wa Ruvu Juu na Ruvu Chini ili kuweza kuwapatia Watanzania na wakazi wa Dar es Salaam maji safi na salama.
Aidha alisema kupitia mpango wa Matokeo Makubwa sasa (BRN), wizara hiyo imejitahidi na kufanya vizuri kwa kuwapatia asilimia 53 ya Watanzania maji safi na salama kutoka asilimia 40.
Zoka ambaye anakwenda Canada kuwa Balozi wa Tanzania aliahidi kuhakikisha kuwa uwepo wake nchini humo, unaipatia maslahi na faida kubwa Tanzania.
“Ni heshima kubwa kupewa nafasi ya kuwa mwakilishi wa nchi yangu katika taifa hili kubwa. Canada imekuwa mshirika mzuri wa nchi yetu, wamewekeza katika miradi mingi ikiwemo gesi na mafuta itakuwa ni jukumu langu kuhakikisha maslahi ya Tanzania yanazingatiwa,” alisisitiza.
Mongella alisema kwa upande wake hana miujiza mingi kwa wakazi wa Kagera ila ataangalia namna ya kushirikiana na wananchi kuboresha masuala ya ulinzi na usalama na alitaja vipaumbele vyake katika mkoa huo kuwa ni ulinzi, usalama, amani na utii wa sheria.
Naye Mapunda ambaye amekuwa RAS wa Arusha alisema kutokana na uzoefu wake wa kufanya kazi katika halmashauri kwa miaka 27, atautumia kwa kushirikiana na jamii jijini Arusha ili kuwapatia maendeleo wakazi wa jiji hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment