Thursday, 13 November 2014

DEWJI AZIDI KUNG'ARA AFRIKA

MFANYABIASHARA maarufu hapa nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’, amezidi kung’ara katika biashara ambako safari hii amejumuishwa kwenye orodha ya mabilionea 55 wa Afrika.


Mo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mjini (CCM), katika orodha hiyo iliyotolewa na Jarida la Ventures Africa, anatajwa kuwa tajiri mdogo zaidi (39), barani Afrika anayemiliki mali zenye thamani ya dola bilioni 2 za Marekani na ametoa ajira 16,800.
Mfanyabiashara mwingine anayelingana umri na Mo, ni Igho Sanomi kutoka Nigeria, aliyeshika namba 38 ambaye ana utajiri unaofikia dola bilioni 1.3 na ametoa ajira kwa watu 1,300.
Kwa mujibu wa jarida hilo, Mo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mohamed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), amefanikiwa kuboresha biashara iliyoanzishwa na familia yake hadi kuwa kampuni kubwa iliyosambaa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Hii ni mara ya pili kwa jarida hilo kutoa orodha ya matajiri barani Afrika huku likieleza bado kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya matajiri kutokuwa na utamaduni wa kutaja mali wanazozimiliki.
Katika orodha hiyo iliyotangazwa na jarida hilo, Mfanyabiashara kutoka Nigeria Aliko Dangote ndiye anayeshika namba moja na pia kwenye orodha hiyo yumo mfanyabiashara kutoka Tanzania, Rostam Aziz, aliyeshika namba 40 akiwa na utajiri unaofikia dola bilioni 1.2 za Marekani na kutoa ajira 1,639.
Ventures Africa, limebainisha kuwa linatoa orodha ya watu matajiri Afrika ili kuwapa changamoto wajasiriamali wadogo wajue historia ya matajiri wakubwa, kwa lengo la kupata hamasa na kuongeza juhudi katika biashara zao.
Kampuni ya MeTL’ inakua kwa kasi ambapo hivi karibuni ilizindua vinywaji vipya mbalimbali ikiwemo Mo bomba, Mo cola, Mo embe na vingine vya aina tofauti kulingana na mahitaji ya jamii.
Dewji, anasema miongoni mwa mafanikio anayojivunia ni kukua kwa kiwanda cha A-One kinachozalisha vinywaji hivyo vipya vilivyoanza kuwa kipenzi kwa watumiaji wake.
Alibainisha kuwa kukua kwa MeTL, kumechangia kuongezeka kwa ajira, kodi na huduma kwa jamii na hivi sasa uzalishaji wa vinywaji hivyo vimetoa ushindani kwa vinywaji vya Coca-Cola na Pepsi.
Alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kufanya kazi kwa saa 22 kwa siku na kuzalisha katoni milioni tatu za vinywaji mbalimbali kwa mwezi.
Jarida la Ventures Africa limeweka wazi kuwa lilitembelea hapa nchini kufanya mazungumzo na Dewji pamoja na kuangalia anavyoendesha biashara zake.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!