Wednesday, 19 November 2014

BOHARI KUU YA DAWA (MSD) YAANZA KUSAMBAZA MADAWA



Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imeanza kusambaza dawa katika hospitali mbalimbali nchini, baada ya kupokea kiasi cha Sh20 bilioni ambazo ni sehemu ya malipo ya deni linaloidai Serikali.


Hata hivyo, kaimu mkurugenzi wa MSD, Cosmas Mwaifani alisema jana kuwa fedha hizo zitapunguza kwa kiasi kidogo tu deni hilo ingawa alisema bohari hiyo haijawahi kukataa kutoa dawa katika hospitali.
“Kama wana fedha za kutosha sisi kwetu hilo si tatizo kwa sababu dawa tunazo. Wakifuata masharti ya ununuzi, tunawapa dawa,” alisema Mwaifani.
Alisema fedha zilizopokelewa tayari zimeshaingizwa katika mzunguko wa ununuzi wa dawa kwa baadhi ya hospitali kwa kufuata vipaumbele.
Kuhusu shehena ya dawa kukwama bandarini, Mwaifani alisema ni kawaida kwa mizigo kukwama kutokana na mchakato mrefu wa utoaji mizigo ambao unahusisha sehemu nyingi za ukaguzi na udhibiti.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Mionzi.
Kauli ya Mwaifani imekuja wakati kukiwa na taarifa kutoka hospitali mbalimbali nchini ambazo watendaji wake wakuu wamedai kwamba hawajapokea dawa kutoka MSD, badala yake wametumia njia mbadala ikiwa ni pamoja na kutumia fedha wanazokusanya kutoka kwa wagonjwa kwa ajili ya kununulia dawa za dharura.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara, Dk Iragi Ngeregeza alikiri kuwapo na upungufu wa dawa katika hosptali yake na kwamba, tatizo hilo limesababishwa na MSD iliyowapelekea kiwango kidogo cha dawa tofauti na walivyoagiza.
“Ni kweli dawa hakuna na ni vigumu kuwa na dawa za aina zote, ila huduma zinaendelea kama kawaida tena madhubuti kwa wagonjwa wa aina zote,” alisema Dk Ngeregeza.
Alisema uongozi wa hospitali hiyo unajitahidi kuhakikisha dawa muhimu kama za upasuaji, wajawazito na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, zinapatikana.
Mkoani Morogoro, mganga mkuu wa hospitali ya mkoa huo, Dk Ritha Lyamuya alisema uhaba wa dawa katika hospitali hiyo si mkubwa kwa kuwa wanatumia nusu ya makusanyo ya mapato kununulia dawa. “Katika hospitali yetu tumejiwekea mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mgonjwa anapoingia hatoki nje ya hospitali kwa ajili ya kutafuta dawa. Ukiacha dirisha la dawa, tumeweka duka jingine la dawa na tutaweka jingine katika korido ya kwenye wodi ili wagonjwa wapate urahisi,” alisema Dk Lyamuya.
Mkoani Mtwara, mfamasia wa Hospitali ya mkoa huo, Flora Makenya alisema hakuna uhaba mkubwa wa dawa kwa kuwa za dharura zipo za kutosha. “Hali ya dawa sio nzuri kama ilivyokuwa awali, isipokuwa kwa wagonjwa wa dharura dawa zipo. Tunazinunua kutokana na fedha tunazokusanya hapa,” alisema Makenya.
“Kwa matumizi ya dharura zipo na tunaweka kipaumbele kwenye vifaa vya kutolea huduma, tofauti na ilivyo kwenye dawa za kutuliza maumivu kama paracetamol ambazo hatuwezi kusema tunazihifadhi kwa ajili ya dharura.”
Alisema kwa kawaida Serikali huingiza fedha kwa ajili ya kuwezesha hospitali hiyo kununulia dawa na mara ya mwisho walipokea fedha hizo mwanzoni mwa mwezi huu.
Katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga (Bombo), mganga mkuu wa mkoa, Dk Asha Mahita alisema huduma za utoaji wa dawa unaendelea kama kawaida. “Zipo za kutoka MSD, lakini pale inapotokea upungufu wakati zikisubiriwa nyingine tunatumia mafungu ya michango ya wagonjwa kununua dawa,” alisema Dk Mahita.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!