Friday, 7 November 2014

AJALI YA TRENI NA BASI ILIYOPOTEZA MAISHA YA WATU 12 WILAYANI KILOMBERO, WATATU WATAMBULIWA



MATUKIO ya ajali za barabarani nchini yameendelea kuteketeza maisha ya Watanzania, baada ya jana watu 12 kufa papo hapo katika ajali iliyohusisha basi na treni katika makutano ya reli eneo la Kiberege, wilaya Kilombero mkoani Morogoro.



Watu 40 walijeruhiwa katika ajali hiyo.
Ajali hiyo, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paul, ilitokea jana majira ya saa 9:15 alasiri ikihusisha basi aina ya Scania lenye namba za usajili T 725 ATD, mali ya kampuni ya Aljabry na treni mali ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Wakati basi hilo lilikuwa likitoka Morogoro kwenda Ifaraka, treni ilikuwa inatoka Mbeya kwenda Dar es Salaam. Kamanda Paul alisema dereva wa basi hilo ambaye hakufahamika jina mara moja hakuwa makini wakati akivuka katika eneo hilo, hali iliyosababisha gari alilokuwa analiendesha kugongwa kwa nyuma na treni.
Alisema wote waliokufa papo hapo ni abiria wa basi, kati yao sita wakiwa ni wanaume, wanawake wanne na watoto wawili wenye umri wa kati ya miaka 5 hadi 6.
Baadhi ya majeruhi waliondolewa eneo la tukio na wasamaria na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Francis ya mjini Ifakara.
Hata hivyo, kwa upande wa waliokufa, watatu wametambuliwa kuwa ni Flugencia Lusangila (60) na Albeta Lusangila (62), wakazi wa Ichonde, Mang’ula wilayani Kilombero na Joseph Kuzwila (34) mkazi wa Dar es Salaam.
Mara baada ya kusababisha ajali, dereva alikimbia na kwamba Polisi inaendelea kumtafuta sambamba na kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!