Thursday 2 October 2014

MAHAKAMA KUU YAZUIA TANESCO KUSIMAMIA MITAMBO TEGETA


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imeamuru Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong na Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (Tanesco) kutoingilia umiliki, usimamizi na utawala wa Mitambo ya ufuaji umeme iliyopo Tegeta, Dar es Salaam hadi hapo uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya msingi utakapotolewa.



Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions Limited (PAP) zinazomiliki mitambo hiyo, zilifungua kesi kuhoji uhalali wa uamuzi wa Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) dhidi ya Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) na Martha Renju (anayedaiwa kuwa msimamizi wa mali zake).
Katika uamuzi wa mahakama ulioandikwa na Jaji Fauz Twaib na kusomwa kwa niaba yake na Jaji Amri Hamisi Msumi, taasisi hizo zimezuiwa kubughudhi IPTL na PAP; zinazomilikiwa na Harbinder Singh Sethi.
Katika uamuzi huo uliotolewa juzi na mahakama mbele ya Sethi pamoja na Mkurugenzi wa SCB-HK, Kieren Day, Jaji Twaib aliamuru Tanesco kutofanya biashara yoyote na SCB-HK au Martha Renju kwa niaba ya IPTL / PAP bila ya idhini ya kimaandishi kutoka kampuni hiyo ya kufua umeme.
"Wadaiwa kwa pamoja wanazuiliwa kufanya utekelezaji wa uamuzi uliotolewa katika chombo cha kimataifa cha ICSD,” ilisema sehemu ya uamuzi huo.
Tanesco ambayo iliwakilishwa na Wakili wake Urassa, pia imezuiwa kulipa kwa SCB-HK na Martha Renju malipo yoyote wanayostahili IPTL / PAP bila ya idhini ya maandishi kutoka kwa IPTL / PAP.
Mahakama pia imezuia Tanesco kutekeleza au kukubaliana na au kutekeleza uamuzi wa ICSID, na kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya msingi.
Jaji Twaib alitupilia mbali hoja ya mwanasheria wa SCB-HK, Charles Morrison, aliyedai Mahakama Kuu ya Tanzania haipaswi kusikiliza na kutoa uamuzi juu ya ombi hilo kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa ICSID. Hata hivyo Jaji Twaib alisema,
"Nashindwa kuelewa ni jinsi gani serikali ya Tanzania, ambayo si sehemu ya kesi hii, itakuwa imevunja Mkataba wa Washington kwa sababu tu ya wananchi wake wawili ambao ni wafanyabiashara binafsi, wametafuta amri ya kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa ICSID kwa misingi ya udanganyifu.“
Katika uamuzi, Jaji anaendelea kunukuliwa akisema, “Sioni ni jinsi gani, kwa kutumia mamlaka yake katika kutoa maagizo hayo, mahakama hii itakuwa inaingilia majukumu ya kimataifa ya Tanzania chini ya Mkataba wa Washington."
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwanasheria wa IPTL/PAP, Joseph Makandege alisema uamuzi huo ni mzuri kwa kwani unawapa nguvu za kuendelea kuzalisha umeme na kuiuzia Tanesco huku mmiliki halali akiwa PAP.

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!