Wednesday 1 October 2014

ALIYEMCHAPA RAILA ODINGA BAKORA ASHITAKIWA

Bwana Lengo Karisa Mudzomba (40) akiwachapa bakora Raila Odinga na Salim Mvurya.


MWANAMUME aliyemshambulia kiongozi wa Cord, Raila Odinga na Gavana wa Jimbo la Kwale, Salim Mvurya ameshtakiwa juzi katika mahakama ya Kwale nchini Kenya.
Mtuhumiwa Lengo Karisa Mudzomba.
Bwana Lengo Karisa Mudzomba (40), alishtakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Kwale, Christine Njagi kwa kuwashambulia viongozi hao wawili na kuvuruga mkutano wao katika soko la Kinango Jumatatu ya Septemba 29, mwaka huu. Baadaye mtuhumiwa aliachiliwa kwa dhamana.
Bw Mdzomba alikiri mashtaka hayo na kuomba mahakama impe muda wa kuomba msamaha kutoka kwa wanasiasa hao. “Nimekubali mashtaka dhidi yangu ila naomba mahakama hii inipe muda wa kuomba msamaha kwani kosa si kosa ila kurudia kosa ndiyo kosa,” alisema Lengo.
Mtuhumiwa huyo alidai atahitaji muda wa wiki mbili kufanya hivyo akisema familia yake iko mbali.
Kiongozi wa mashtaka George Mungai alikubali ombi hilo akisema litatoa fursa kwa waathiriwa kujitokeza.
Mahakama iliamua kutaja kesi hiyo Oktoba 14, 2014 na Bw Mudzomba hakupinga.
Mwajiri wa mshtakiwa, Bi Nassim Issa, alisema alishangazwa na tukio hilo kwani hakulitarajia.
Bi Issa alimtaja Bw Mdzomba kuwa mtu mpole, mnyenyekevu na mwenye akili timamu.
“Nimekuwa nikiishi naye kama mfanyakazi wa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu na hakuonyesha dalili zozote za upungufu wa kiakili,” alisema Bi Issa.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 60 alifichua kuwa siku ya tukio hilo alimkuta Bw Mdzambo ameketi nje ya nyumba yake akionekana mwenye hasira nyingi.
Na alipomuuliza ni kwa nini hakwenda mkutanoni, alimjibu kwamba alikuwa huko lakini maneno aliyosikia hayakumfurahisha.
“Walikuwa wanazungumza kuhusu Okoa Kenya. Ni Kenya gani ambayo wanataka kuokoa ilhali Kenya ni taifa huru na wananchi wanaishi katika maisha ya dhiki?” Bi Issa alimnukuu.
Kauli hiyo ni tofauti na ya Kamishna wa Kaunti ya Kwale Bw Moses Ivuto ambaye aliwaambia wanahabari kuwa Bw Mdzomba alitenda kitendo hicho baada ya kusukumwa na mtu asiyemjua.
Bw Ivuto alisema Mudzomba alikuwa ameenda katika mkutano huo na matumaini ya kupata kitu kidogo lakini hakupata chochote.
“Kulingana na maelezo yake kuna mtu aliyemsukuma ndipo akaamua kulipiza kisasi kwa kuwacharaza wawili hao kwa bakora yake,” alisema Bw Ivuto.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!