Monday, 1 September 2014
WATENDAJI WENYE TAMAA KUKIONA!
RAIS Jakaya Kikwete amesema itatengenezwa dawa ya wadaiwa sugu wa maji hususan taasisi za Serikali, walipe ankara zao kwa wakati. Alisema sasa halmashauri zina fedha nyingi kuliko wakati wowote kutokana na ongezeko la kukusanya kodi; jambo alilotaka fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitumike kama ilivyokusudiwa.
Kikwete ambaye hata hivyo hakufafanua zaidi dawa inayoandaliwa dhidi ya taasisi husika, alitoa kauli hiyo juzi kwenye mkutano wa hadhara mjini Mpwapwa ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Dodoma.
“Fedha zinazoletwa kwenye halmashauri hakikisheni zinatumika kama ilivyokusudiwa na si kuachwa ziliwe na watu wachache wenye tamaa,” alisema.
Alisisitiza halmashauri kuhakikisha hatokei mtu wa kutafuna fedha hizo zinazokwenda kwenye maendeleo.
Kauli ya Kikwete ilitokana na taarifa iliyotolewa kwenye mkutano huo juu ya deni ambalo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linadai taasisi mbalimbali zikiwemo wilayani Mpwapwa na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwemo maji.
Kutokana na madeni hayo, katika mkutano wa hadhara, Wizara ya Maji imeahidi kulipa deni la Sh milioni 82 zinazodaiwa na Tanesco Wilaya ya Mpwapwa kuwezesha upatikanaji maji.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alisema hatua ya taasisi nyingi za Serikali kushindwa kulipa madeni yao, inazorotesha upatikanaji wa maji kwenye taasisi nyeti kama vile hospitali.
Alisema tatizo lililopo ni kwamba wanaolipia huduma ya maji ni wananchi wa kawaida lakini taasisi za Serikali kama vile Polisi, Magereza, Chuo cha Ualimu zimekuwa zikilimbikiza madeni yao na kufanya Tanesco ishindwe kutoa huduma kwa ufanisi.
Alisema Tanesco wamekuwa hawalipwi kwa muda mrefu na wamekuwa wakitafuta njia za kufanya watumiaji walipe madeni yao ikiwemo kukata huduma ya maji
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment