WANAWAKE wa Kijiji cha Michese kata ya Mkonze Manispaa ya Dodoma wamelalamikia tatizo la maji ambalo linawafanya kila siku kuwaamsha wanaume wao usiku wa manane kuwasindikiza kusaka maji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi habari hizi mmoja wa wakazi hao Maria Abeli mkazi wa Kitongoji cha Mbuyuni alisema kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa huduma ya maji na wanawake wamekuwa wakitumia muda mwingi kwa ajili ya kutafuta maji badala ya kushiriki shughuli nyingine za maendeleo.
Alisema wamekuwa wakiamka saa 12 alfajiri kwenda bombani kwa ajili ya kuwahi foleni kutokana na maji hayo kutolewa kwa mgawo.
“Hapa maji yanatolewa kwa mgawo ikifika saa nne asubuhi yanakatika kwa hiyo usipowahi foleni ya usiku unakosa hata maji ya kunawa uso,” alisema.
Alisema kutokana na tatizo hilo wamekuwa wakiamka usiku wa manane na kusindikizwa na waume zao ili kuepuka na vitendo vya ubakaji ambavyo wamekuwa wakifanyiwa wanawake hasa wanapokuwa peke yao.
Mkazi huyo alisema kutokana na kero hiyo baadhi ya familia hivi sasa wameamua kwenda kuchota maji hayo mjini kwa kutumia magari ambako toka hapo kijiji hadi mjini kuna umbali wa kilometa saba na kulazimika kulipia nauli ya 500 kwa ndoo ya lita 20.
Kwa upande wake, Zipora Chijaka alisema wanawake wa kijiji hicho pia wameingia katika migogoro kati yao na waume zao kutokana na kero hiyo ya kuamka alfajiri kwa ajili ya kuwahi foleni hiyo ya maji.
Alisema wapo wanawake waliotengana na waume zao kutokana na kupigwa pindi wanaporudi majumbani hawana maji, kwa kufikiriwa hawakuwepo kwenye utafutaji wa maji, bali walikuwa nyumba ndogo.
Alisema kama hali hiyo isipotatuliwa na kuna hatari hata ya kutokea mauaji, kwani mwaka jana baadhi ya vijana waliwahi kuwavamia wakiwa bombani kwa madai wanaharibiwa kazi yao.
“Tulishawahi kuvamiwa tukiwa bombani na kundi la vijana waliokuwa na mapanga wakidai kuna tunawaharibia kazi zao za usiku, tunaomba serikali itusaidie katika hili la upatikanaji wa maji ya uhakika ili na sisi tuwe na amani,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho Sostenes Matahi, alisema tatizo la maji kutolewa kwa mgawo linatokana na kuongezeka kwa wakazi katika eneo hilo.
“Ni kweli wanaume wamekuwa wakiwasindikiza wake zao ili kuwalinda wake zao wasidhurike na vibaka hao ikiwemo pia na hata na wanyama wakali wanaotembea usiku huo wa manane,” alisema.
Pamoja na hayo, alisema Serikali ya kijiji imetekeleza mradi wa kujenga tangi la maji kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ambapo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kujaza lita 9,000, na kuwawezesha pia wakazi hao kuvuta mabomba ya maji hadi majumbani mwao na hatimaye kuondokana na kero hiyo.
1 comment:
kazi kwelikweli
Post a Comment