Monday, 8 September 2014

WALIOFARIKI AJALINI WATAMBULIWA

Watu 35 waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha magari matatu eneo la Sabasaba Wilaya ya Butiama mkoani Mara wametambuliwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Philip Kalangi alisema marehemu hao wameshatambuliwa na kwamba majeruhi 19 walio katika hali mbaya wamehamishiwa Hospitali ya Bugando Mwanza kwa matibabu zaidi akiwamo mwandishi wa habari wa gazeti la Raia Tanzania, Pendo Mwakyembe.
Alisema vilevile vifo vimeongezeka hadi kufikia watu 37 baada ya majeruhi mmoja kufariki jana.
Dk Mwakyembe
Katika hatua nyingine, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema Serikali inatarajia kufanya operesheni nchi nzima kuwabaini madereva wasio na sifa, hatua itakayopunguza ajali ambazo zinachukua maisha ya Watanzania wengi.
Akizungumza jana baada ya kutembelea eneo la tukio, Dk Mwakyembe alisema kutokana na hali hiyo, itafanyika operesheni kwa miezi sita nchini nzima kuwabaini wazembe.
Pia alisema Serikali itazifanyia ukaguzi kampuni zote za usafirishaji nchini ili kubaini iwapo mabasi yanayosafirisha abiria yanakidhi vigezo vya kufanya biashara hiyo.
Waziri huyo alisema imebainika kuwa ajali nyingi zinazotokea zinasababishwa na madereva walevi, hivyo amewaomba wananchi kutoa taarifa wanapombaini dereva wa aina hiyo.
“Nawaomba wananchi kutoa taarifa kuhusu madereva wanaotumia viroba wakati wanaendesha ili hatua za haraka zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kufungia leseni zao,” alisema.
Dk Mwakyembe alieleza kwamba baadhi ya mabasi yamechakaa kiasi ambacho hayawezi kutumika kusafirisha abiria.
Akizungumzia ajali iliyotokea Ijumaa, alisema kuwa Serikali itafanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo chake ingawa ilikwishaelezwa kuwa magari hayo yalikuwa katika mwendo wa kasi. Aliongeza kuwa Kampuni za Mwanza Coach na J4 ambazo mabasi yake yalipata ajali leseni zao za biashara zitafutwa kwa muda wakati mamlaka husika zikiendelea na uchunguzi.
Kamanda Mkuu Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga alisema Serikali haitaendelea kuwavumilia madereva wasiofuata sheria za usalama barabarani na kwamba dereva pekee mwenye leseni kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ndiye atakayeruhusiwa kuendesha.
Aliwataka madereva wote wenye leseni bandia na wasio na leseni kwenda kusoma katika vyuo vinavyotambulika na kupata vyeti.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!