Uchunguzi wa mwili wa marehemu Liberatus Matemu(55), aliyefia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akidaiwa kupigwa na askari polisi wa Kituo cha Stakishari umeshindwa kufanyika jana baada ya kutokea utata wa nani anatakiwa kulipa gharama za matibabu Sh260,000.
Utata huo ulijitokeza baada ya madaktari, polisi na ndugu wa marehemu kufika katika hospitali hiyo kwa lengo la kufanya uchunguzi lakini wakashindwa kufanya hivyo baada ya Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (Moi), kutaka ilipwe kiasi hicho ikiwa ni gharama za matibabu ya marehemu.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipopigiwa simu jana ili aeleze kama polisi watalipa gharama hizo alitaka apigiwe simu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Mary Nzuki aliyekuwa akishughulikia suala hilo.
Alipopigiwa Kamanda Nzuki,simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Naye Ofisa wa Idara ya Mawasiliano Moi, Patrick Mvungi alipotakiwa kuzungumzia gharama hizo alisema hana taarifa na kuomba apewe muda ili alifuatilie.
Akizungumzia suala hilo, Mwanasheria wa familia ya marehemu, Benedict Baligiye alisema jana kwamba, uchunguzi umeshindwa kufanyika kwa sababu ya kuwapo kwa mvutano kati ya polisi na familia hiyo kuhusu nani anayetakiwa kulipa gharama hizo za MOI.
“Watu wote wanaotakiwa kufanya uchunguzi walikuwa wamefika Muhimbili tangu saa 3.00 asubuhi lakini wameondoka baada ya mvutano huo,” alisema.
Alisema ili uchunguzi huo ufanyike Moi wanatakiwa kutoa faili la marehemu Matemu alipokuwa mgonjwa kwa timu ya watu wanaofanya uchunguzi.
Baligiye alisema uongozi wa Moi umekataa kutoa faili hilo kwa sababu bado haujalipwa fedha hizo za matibabu.
Alisema wanafamilia hao wanasema polisi ndiyo wanatakiwa kulipia gharama hizo kwa sababu Matemu alikufa akiwa mikononi mwao.
“Kwa hiyo ninachokifanya ni kutumia busara kuishauri familia hiyo kuona umuhimu wa kulipa gharama hizo,” alisema.
Juzi, Kamanda Kova alitangaza jopo la wapelelezi kuchunguza kifo cha marehemu huyo baada ya maiti yake kukataliwa na ndugu zake.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment