Monday, 22 September 2014

TWENDENI UWANJANI TUKAONE TUNAPOKOSEA"


Nimekuwa shuhuda wa muda mrefu wa mechi za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Katika kipindi chote cha kushuhudia mechi hizo tangu miaka ya tisini, nilichokiona na kinaendelea kutokea ni wachezaji wetu kuwa na upungufu katika mambo ya msingi ya soka. Hatuhitaji kufanya tathmini ya kina kubaini hilo, nenda uwanjani kashuhudie mechi za Ligi Kuu Bara iliyoanza Jumamosi iliyopita na jaribu kuangalia mambo ya msingi ya soka kwa wachezaji wetu.
Mambo ya msingi kama kukokota mpira, kupokea mpira, kutuliza kwa usahihi, kupiga pasi, kupiga mpira kwa kichwa, kuulinda mpira, kupiga mashuti, kunyang’anya mpira, kurusha mpira, upigaji wa faulo, kuokoa mpira, upigaji wa kona, mbinu za ushambuliaji, ulinzi na nyingine.
Kwa haraka haraka inaweza kuwa ngumu kunielewa maana yangu, lakini ninapozungumzia kukokota mpira ni wazi mchezaji anayekokota mpira vizuri huwa na uwezo mkubwa wa kuanzisha mashambulizi kwa kasi au kutengeneza mazingira ya kuokoa au kuweka mazingira ya kupiga shuti au kujitengenezea mazingira mazuri ya kupiga pasi, pia mchezaji anayekokota mpira vizuri huisumbua ngome ya timu pinzani kila anapokuwa anakuja na mpira.
Zipo aina tofauti za kukokota mpira, mchezaji anaweza kutumia sehemu ya ndani au ya nje ya mguu kukokota mpira na hatakiwi kukokota mpira huku akiangalia chini.
Hali kadhalika katika soka kama huwezi kutuliza mpira vizuri unapopewa lazima utapoteza mipira mingi.
Pia katika soka kupiga pasi ni muhimu kwa kila mchezaji uwanjani. Zipo aina tofauti za upigaji wa pasi, zipo pasi za kupiga kwa nguvu, pasi za kupenyeza, pasi za kawaida, pasi za kupiga sehemu ya ndani ya mguu, pasi za kukata kwa kupiga kwa sehemu ya nje ya mguu, pasi ndefu, pasi fupi na krosi. Pasi zote hizo zina aina ya upigaji wake ili kupata kasi sahihi.
Vilevile kupiga mpira kwa kichwa ni muhimu kwa washambuliaji ambao wanatakiwa kuunganisha krosi za juu, kwa mabeki ambao wanaokoa krosi za juu, kwa viungo wanaopokea mipira ya juu iliyookolewa na mabeki kwa ajili ya kuipeleka sehemu sahihi kwa kichwa pia.
Ni wazi mchezaji soka mzuri lazima ajue kuulinda mpira. Kuulinda mpira kunahitaji mchanganyiko wa kuwaza ya mbele, stamina na nguvu ya mwili. Kuulinda mpira ni muhimu kwa washambuliaji kwani wanatakiwa kutengeneza na kulinda nafasi ili wapokee mpira, pia ni muhimu kwa mabeki na viungo ili wasipokonywe mpira na kuanza kuutafuta.
Ukiacha njia ya kufunga kwa kutumia kichwa, msingi wa kupiga mashuti ndiyo njia sahihi ya kufunga mabao. Ili kuwa na ujuzi sahihi wa kupiga mashuti kuna mambo mawili ya kuzingatia ambayo ni nguvu na usahihi.
Katika msingi wa soka wa kunyang’anya mpira hapa zipo njia tofauti za kunyang’anya mipira, mojawapo ni njia ya kulala au kumuibia mpinzani wako. Katika soka la sasa kila mchezaji uwanjani anatakiwa kujua kunyang’anya mpira.
Pia kurusha mpira ni msingi muhimu wa soka, zipo mbinu za kutumia mpira wa kurusha kama ilivyo katika kupiga faulo au mipira ya kona.
Katika soka kuokoa siyo kubutua mpira mbele, ingawa wengi huiona hiyo ndiyo njia ya kuokoa, lakini uokoaji mzuri ni kuulinda mpira na kupiga pasi, kuokoa kwa kupasiana huonyesha wachezaji wa timu husika wanajiamini na pia hutumia njia hiyo kuanzisha mashambulizi tangu nyuma.
Ukienda uwanjani kushuhudia mechi za Ligi Kuu Bara utaona wachezaji wetu walivyo na upungufu katika mambo hayo ya msingi ya soka niliyoyataja na ndiyo maana nawashauri Watanzania tujitokeze viwanjani kushuhudia mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na kuona wapi Tanzania tunapokosea katika soka letu na hivyo kushindwa kufanya vizuri kimataifa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!