MKUU wa kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya nchini, Godfrey Nzowa amesema mawasiliano baina ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yamefanikisha kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya hapa nchini.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam, Nzowa ambaye pia ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) alisema wanafanyakazi kama timu kwa nchi za Afrika Mashariki na duniani kuhakikisha wanaweka mipango madhubuti ya kudhibiti uingizaji na uuzaji wa dawa hizo.
Akitoa mfano, alisema katika kipindi hiki ni vigumu kwa wauzaji kupata hata kilo moja hivyo wanalazimika kutafuta kwa gharama kubwa zaidi.
“Mawasiliano ya pamoja baina ya nchi wanachama yamefanikisha kudhibiti tatizo hilo maana hivi sasa wauzaji wanahangaika kutafuta hata nusu kilo na hata wakipata inakuwa ni gharama kubwa inaweza kuuzwa kati ya sh milioni 45 hadi sh milioni 60,” alisema kamanda Nzowa.
Alisema kuwa mawasiliano hayo ni ya dunia nzima na iwapo kuna dawa zinazopenya na kuingia nchini zinakuwa zimepitishwa njia za panya.
Alisema kuwa wauzaji na waingizaji hao wamejaribu kubadili mfumo wa utengenezaji kwa kuweka katika vibashirifu lakini wabainika na kudhibitiwa.
“Hivi sasa tunapambana kama ulimwengu katika suala hili… hata Mei mwaka huu tulikuwa na mkutano Itali wa kimataifa huko ndiyo tunaelezana mipango tunayofanya na hatua zipi tumechukua,” alisema.
No comments:
Post a Comment