Wednesday, 3 September 2014

TUME: POLISI BADILIKENI



Ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Germanus Kyafula akionesha vitabu vya mwongozo wa Polisi na mambo 101 unayohitaji kuyafahamu kuhusu Polisi unaogopa kuyauliza, wakati akizungumza na waandishi Dar es Salaam jana kuhusu Tanzania kuongoza nchi za Afrika katika Maboresho ya Utoaji Haki za watuhumiwa na Mahabusu na Utekelezaji wa miongozo ya Luanda kuimarisha Haki za Binadamu nchini. Wengine ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo, Alexander Hassan na Mkurugenzi Idara ya Huduma za Kisheria, Nabor Assey. (Picha na Yusuf Badi).

BAADHI ya askari Polisi wa Tanzania, wametajwa kushiriki vitendo vya kunyanyasa raia wakati wa kukamata watuhumiwa, kuwahoji na wakati wa kuwaweka ndani.
Utafiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), kwa kushirikiana na Mtandao wa Wataalamu wa Masuala ya Kipolisi Afrika (APCOF), umebaini hilo na kutoa mapendekezo yake kwa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR).



Akielezea hali hiyo katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jana, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa tume hiyo, Nabor Assey, alisema baada ya matokeo ya utafiti huo, tume hiyo ya Afrika iliamua kutengeneza miongozo ya kubadilisha hali hiyo.
“Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ilianzisha mchakato wa kuandaa miongozo ya namna ya kukuza na kulinda haki za binadamu nyakati za kukamatwa kwa watuhumiwa, kuwekwa ndani ya mahabusu za Polisi na wakiwa mahabusu za Magereza,” alisema.
Miongozo hiyo kwa mujibu wa taarifa ya Tume iliyotolewa jana, iliridhiwa katika Mkutano Mkuu wa 55 wa tume hiyo ya Afrika, uliofanyika Luanda, Angola Mei, mwaka huu na kupewa jina la Miongozo ya Luanda, ambapo Tanzania iliteuliwa kuwa miongoni mwa nchi tano za mwanzo Afrika, zilizopewa kipaumbele katika utekelezaji wa miongozo hiyo.
Nchi nyingine ni Zimbabwe, Malawi, Tunisia na Ivory Coast, ambazo zimetakiwa kuboresha mifumo yao ya haki jinai ili baada ya hapo, itumike kuwa mfano kwa nchi zingine za Afrika.
Utesaji
Kwa mujibu wa utafiti huo, ukamataji unaofanywa na vyombo vya dola hususan Jeshi la Polisi nchini, mara nyingi unakiuka haki za binadamu, kwani imebainika kwamba kumekuwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa, ambayo huambatana na vitendo vya utesaji wa watuhumiwa.
“Utesaji huo hufanywa wakati wa mahojiano kwa lengo la kushinikiza watuhumiwa kukiri makosa. Takwimu za utafiti zilizofanywa na tume kwa nyakati tofauti, zinaonesha pia kwamba yapo malalamiko mengi yanayopokewa kutoka kwa watuhumiwa na wafungwa, kuhusu kubambikiwa kesi na polisi,” ilieleza taarifa hiyo.
Utesaji mwingine wa raia, umetajwa kuwa ni muendelezo wa athari zinazotokana na matumizi ya nguvu na ukiukwaji wa haki za binadamu katika ukamataji, wakati wa kuhoji mtuhumiwa na hata kumshikilia bila sababu za msingi.
“Athari za watu kushikiliwa vizuizini pasipo ulazima ni … watuhumiwa wa uhalifu kupata magonjwa ya kuambukizwa kutokana na msongamano, kupata ulemavu na hata kufa kutokana na mateso,” imeeleza taarifa hiyo.
Athari za kiuchumi ambazo zinaendeleza mateso kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni pamoja na familia nyingi kuathirika kwa kukosa mahitaji muhimu kama vile chakula, elimu kwa watoto, matibabu na mengine kutokana na watafutaji kushikiliwa vizuizini kwa muda mrefu.
Ukiukaji Katiba
Taarifa hiyo ya tume, imebainisha kuwa polisi hao wamekuwa wakikiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 13 (6) (e), ambayo inakataza utesaji kwa watuhumiwa, ambapo pia imeelekeza mamlaka za nchi, kutunga sheria kwa minajili hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, polisi hao wameendeleza utesaji kutokana na upungufu katika Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 ya Sheria za Tanzania, kifungu cha 29, kinachokataza ushahidi uliopatikana kwa shinikizo la aina yoyote, kuwa ushahidi halali mbele ya Mahakama.
Upungufu kisheria
Sheria hizo pamoja na kukataza vitendo vya utesaji kwa watuhumiwa wa uhalifu, taarifa hiyo imeeleza kuwa hazitamki wazi ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya mtumishi wa chombo cha dola, ambaye atajihusisha na vitendo vya utesaji wa watuhumiwa.
“Nafuu pekee ya kisheria inayopatikana, ni muathirika wa mateso, kufungua kesi ya madai dhidi ya Serikali,” ilieleza taarifa hiyo.
Upungufu mwingine, umetajwa kuwepo katika Sheria ya Kukazia Haki na Wajibu ya 1994, ambayo imeeleza kuwa ili kesi inayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu isikilizwe, kunahitajika jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika mazingira ya sasa, upatikanaji wa jopo hilo ni mgumu kutokana na upungufu wa maji.
Uwajibikaji
“Hatua zitakazofuata baada ya hapo, zitajumuisha kufanya mapitio ya sheria za jinai zinazohusu ukamataji na ushikiliaji wa watuhumiwa na kubainisha upungufu uliopo na kisha kufanyia marekebisho sheria hizo, ili zikidhi viwango vilivyoainishwa katika Miongozo ya Luanda. “Pale ambapo upungufu utabainika, sheria zitungwe au kurekebishwa ili kubana watendaji wa vyombo vya dola wanaokiuka sheria na miongozo ya kazi zao,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kwa ujumla utekelezaji wa dhati wa sheria zilizopo au zitakazofanyiwa marekebisho au zitakazotungwa upya, utasaidia kuimarisha utawala wa sheria, utu wa mtu, uhuru binafsi wa mtu, amani na utulivu nchini.

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!