Monday 29 September 2014

TANZANIA KUANDIKA HISTORIA MPYA LEO



UPIGAJI wa kura wa kupata Katiba Inayopendekezwa, unatarajiwa kuanza leo mjini Dodoma ambapo Tanzania inaandika historia mpya baada ya miaka hamsini ya uhuru.



Hivyo, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walio bungeni na nje ya Bunge wanatumia nafasi yao ambayo ndiyo msingi uliowaweka kwa kipindi chote, leo wanapiga kura kuikubali au kuikataa kwa njia ya wazi na siri.
Pia wajumbe watakaokuwa nje ya ukumbi huo, wakiwemo watakaokuwa nje ya nchi nao wamewekewa utaratibu wa kupiga kura popote walipo kwa njia ya faksi na intaneti.
Tofauti na wiki iliyopita ambapo aliyewasilisha Rasimu hiyo Inayopendekezwa alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, leo inawasilishwa na Dk Tulia Akson.
Tunaamini wajumbe wako makini kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania ambao wana hamu ya kuona matokeo mazuri ya upigiaji kura ili baadaye waweze kupata nafasi kuweka uamuzi wao itakapokuwa imepitishwa kwa kura hizo ambazo tunaamini zitapigwa kwa amani na utulivu.
Kinachosubiriwa na Watanzania wengi wanaoitakia mema nchi yao, ni kuona theluthi mbili kutoka Tanzania Bara na Visiwani zinapatikana ikizingatiwa kwamba wanaopiga kura ndio hao hao ambao wametengeneza Rasimu hii Inayopendekezwa.
Ikumbukwe kwamba juzi baada ya kupewa nafasi kutoa neno la kuunganisha wajumbe, mjumbe mzee kuliko wote, Kingunge Ngombale Mwiru aliwataka wajumbe wasiangalie mambo binafsi ambayo hayakuwekwa katika Katiba Inayopendekezwa, bali waangalie matakwa ya nchi.
Akasema wananchi wanataka Katiba na kuhadharisha wajumbe hao kwamba wasije wakazuia Katiba bora kwa sababu tu wanataka jambo lingine mbali na matakwa ya Watanzania wanaosubiri kwa hamu kubwa kazi hiyo na pia kwa Rais Jakaya Kikwete aliyewachagua kufanya kazi hiyo, akisema wajumbe wafikirie nchi kwanza na hatima yake.
Akawakumbusha kwamba ili Katiba hii iweze kupita ni lazima ipate theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania Bara na theluthi mbili Zanzibar na hapa maana yake ni kura.
Katika hili, Kingunge amesema kitendo cha kukwamisha rasimu hiyo hakitakuwa na manufaa yoyote kwa Watanzania. Kwa maneno yake, akasisitiza kwamba mkwamo huo kama utajitokeza leo, hautakuwa na tija kwa wafanyakazi, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo na wanawake.
Akasisitiza kuwa yaliyowekwa katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa yanatosha kufanya Tanzania ipige hatua mpya katika miaka hamsini ijayo.
Nasi tunaamini maneno ya Mzee Kingunge ni wosia tosha kwa wajumbe na tunawatakia uamuzi ulio na tija kwa Watanzania kwani kura zao bila kujali njia zitakazotumika iwe ni kwa njia ya siri au wazi, nia ni moja ya kuleta kile kinachosubiriwa na wananchi wanaofuatilia mchakato mzima kuanzia kuanza kwake hadi leo wanapohitimisha kwa kura.
Baada ya hapo, tunaikaribisha rasimu hiyo iingie mitaani ambapo kwa busara zile zile, zitatumika kwa Watanzania pia kuiamulia ili baadaye ipatikane Katiba iliyokusudiwa ambayo tunaamini imejibu maswali ya makundi yaliyokuwa yamesahaulika siku nyingi katika Katiba hii iliyopo kama yalivyoainishwa na Mzee Kingunge.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!