RASIMU ya Tatu ya Katiba mpya, inatarajiwa kuwekwa hadharani Jumatatu ijayo, wakati Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, itakapokuwa ikiwasilisha rasimu hiyo kwa wajumbe wa bunge hilo.
Ratiba ya shughuli za Bunge Maalumu la Katiba iliyopatikana jana bungeni hapo, imeonesha kuwa Sekretarieti ya Kamati ya Uandishi, ilipaswa kukamilisha kuandika Ibara za Rasimu hiyo juzi.
Kuanzia jana, mpaka Jumamosi ya wiki hii, ratiba hiyo inaonesha Kamati ya Uandishi inatakiwa kufanya kazi ya kuandika Rasimu hiyo na kuikabidhi Kamati ya Uongozi Jumapili wiki hii.
Baada ya kukabidhiwa kwa Kamati ya Uongozi, Jumatatu Rasimu hiyo itawasilishwa bungeni na baada ya kuwasilishwa, wajumbe watapewa muda wa kutafakari Rasimu hiyo ya Katiba kuanzia siku hiyo na kesho yake.
Jumatano na Alhamisi wiki ijayo, mjadala wa Rasimu ya Tatu ya Katiba mpya utaanza bungeni pamoja na uhakiki wa Ibara zake kisha Kamati ya Uandishi itarejea kibaruani kufanya marekebisho ya mwisho ya Ibara za Rasimu ya Mwisho ya Katiba.
Jumamosi ya wiki ijayo Septemba 27, Kamati ya Uandishi itawasilisha Rasimu ya Mwisho ya Katiba bungeni, ambapo Jumapili kamati za Bunge Maalumu la Katiba, zitajielimisha kuhusu Rasimu ya Mwisho ya Katiba na taratibu za upigaji kura.
Kura ya kupata Katiba inayopendekezwa, kwa mujibu wa ratiba hiyo, inatarajiwa kuanza kupigwa kuanzia Jumatatu ya Septemba 29, mpaka Oktoba 2, mwaka huu.
Wakati mchakato huo ukiwa katika hatua za mwisho, ule uoga wa kukosekana kwa theluthi mbili za kura kutoka Tanzania Bara za Zanzibar, uliosababishwa na kutokuwepo kwa baadhi ya wajumbe kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umeanza kuondoka.
Tayari Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro, ameshatoa tamko kuonesha kuwa wajumbe wa Ukawa, waliosusa wakitarajia kukwamisha kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa, hawatakuwa na athari.
Kwa mujibu wa Dk Migiro, idadi ya wajumbe wote walikuwa 630, na Ukawa waliosusa ni 130 tu ambao ni sawa na asilimia 21 ya wajumbe wote.
Kwa maana hiyo wajumbe waliobaki ni 500, sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote ambao ni zaidi ya theluthi mbili tayari. Dk Migiro aliweka wazi kuwa wajumbe wanaotoka Tanzania Bara ni 348 na kati yao, 125 wanatoka kundi la 201.
Kwa Zanzibar, takwimu hiyo inaonesha wapo wajumbe 152 ambao kati yao 64 wanatoka kundi la 201.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment