Thursday 25 September 2014

RAIS KIKWETE AWA SAUTI YA AFRIKA UN



MABADILIKO ya tabia nchi duniani yanahatarisha uhai na maendeleo ya binadamu, ikiwemo kurudisha nyuma au kufuta kabisa maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyokwishapatikana.



Rais Jakaya Kikwete aliyasema hayo juzi jijini hapa wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo aliwakilisha msimamo wa bara zima la Afrika kuhusu suala zima la tabia nchi.
Kikwete ametahadharisha kuwa kama hali iliyopo sasa hivi haitashughulikiwa, madhara yake yatakuwa makubwa hivyo dunia inapaswa kuchukua hatua za kukabiliana na tabia nchi.
Alisema Afrika inaamini kuwa hali hii inaweza kubadilishwa kwa sababu wazalishaji wakubwa wa hewa ya ukaa ni nchi zilizoendelea ambazo zina teknolojia, ujuzi wa kiufundi, na uwezo wa kifedha kuchukua hatua zinazostahili.
"Sote tunajua kuwa hiki ndicho kimetamkwa na Mkataba wa Kyoto na itifaki zake na tunachosisitiza hapa ni kuwa, makubaliano haya yaheshimiwe na kutekelezwa," akasisitiza.
Pamoja na mambo mengine, Mkataba wa Kyoto umezitaka nchi ambazo zinazalisha kwa wingi hewa ya ukaa, kuchukua majukumu zaidi ya kupambana na athari za tabia nchi.
Katika utaratibu huo, nchi za Afrika zinachangia kiasi kidogo sana cha hewa ya ukaa na uchafuzi wa mazingira kwa ujumla. Mkutano huo kuhusu tabia nchi uliongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki -moon.
Mapema akihutubia Baraza la UN, Rais Baraka Obama wa Marekani alisema kuwa tishio la tabia nchi ni la dunia nzima na kuelezea kuwa madhara ya tabia nchi yanaongezeka haraka kuliko hata hatua zake za kukabiliana nayo na hivyo dunia inatakiwa kuchukua hatua za haraka na kuahidi kuwa Marekani itazisaidia nchi zinazoendelea kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Viongozi wakuu duniani wamekwishawasili hapa ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitarajiwa kuanza kusikiliza hotuba na misimamo ya nchi wanachama kwa siku nne kuanzia jana na mijadala inatarajiwa kuanzia Jumatatu ijayo.
Masuala makubwa yatakayojadiliwa katika kikao cha Baraza Kuu la UN mwaka huu ni pamoja na kuzungumzia changamoto mbalimbali duniani zikiwemo za umaskini, njaa, usalama na mabadiliko ya tabia nchi. Rais Kikwete jana alitarajiwa kuhutubia baraza hilo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!