Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango), Bi Joyce Mkinga (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati alipokuwa akitoa taarifa ya kufanyika kwa Mkutano wa Maafisa Mipango unaotarajiwa kufanyika Mwezi wa Oktoba mwaka huu. Kulia ni Mchumi Mkuu (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango), Bw. Omary Juma.
………………………………………………
NA SAID MKABAKULI
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ipo katika maandalizi ya mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango unatarajiwa kufanyika Oktoba 2014 jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na usimamizi wa uchumi na mipango hapa nchini.
Mkutano huu ambao niwa kitaalamu unawakutanisha wataalamu mbalimbali kutoka tasnia za mipango, uchumi, takwimu na maendeleo, wenye wajibu wa kusimamia uchumi na mipango ambao hukutana kwa ajili ya kujadili na kubadilishana uzoefu juu ya sera, mipango na kujenga mtandao wa masuala ya maendeleo ya kitaaluma.
Mkutano huu unatoa fursa kubwa ya kuwakutanisha kwa pamoja wataalamu hao na kujenga uelewa wa pamoja juu ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Serikali. Pia hutoa fursa za kujadiliana kwa pamoja juu ya mafanikio na njia za kukabiliana na changamoto kwa kubadilishana uzoefu na ujuzi kwenye masuala hayo. Mkutano huo ni muhimu katika kuimarisha utendaji kazi wa kada hizi kwa minajili ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Kwa kutilia mkazo masuala mbalimbali ya kimaendeleo yanayojitokeza hivi sasa, mkutano wa mwaka huu utajikita katika kujadili masuala yafuatayo;
i) Maendeleo ya Tasnia ya Wapanga Mipango (wachumi, maafisa mipango na watakwimu);
Mkutano utajadili fursa, na changamoto zilizopo katika kuleta maendeleo katika nchi. Huko nyuma kada hizi zilikuwa zinaratibiwa na iliyokuwa Wizara ya Mipango Uchumi na Uwezeshaji. Kwa sasa watakuwa chini ya uratibu wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango. Hatua hii itarahisisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya nchi.
ii) Maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2015/16 – 2020/2021);
Utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Maendeleo 2011/12 – 2015/16) unaendelea na tayari Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango imeanza kufanya mapitio ya utekelezaji wake ili kujua mafanikio na changamoto. Hivyo, katika mkutano huo wapanga mipango wanaandaliwa waweze kuanza kufanya maandalizi kwa ajili ya Mpango wa Pili wa Maendeleo (2015/16 – 2020/21).
iii) Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma;
Serikali imeandaa mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika sekta ya Umma, lengo likiwa kuimarisha utendaji, ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma zilizotengwa kwa ajili ya miradi na program za maendeleo.
iv) Jinsi ya Kujiandaa na Uchumi wa Gesi
Mkutano utajadili ni kwa jinsi gani Tanzania inajipanga kufaidika na rasilimali ya gesi asilia. Kwa kifupi masuala ya yanayohusu uwekezaji katika gesi asilia, usimamizi na jinsi ya kutumia rasilimali na menejimenti ya mapato yatokanayo na gesi, pamoja na ushiriki wa wananchi katika fursa mbalimbali zinazotokana na ujio wa gesi hiyo. Utayarishaji wa wataalam katika eneo hilo la gesi husani vyuo vya ufundi, vyuo vikuu na kadhalika.
Washiriki wa mkutano huu ni pamoja na wakurugenzi wa sera na mipango, maafisa mipango kutoka kwenye wizara, Serikali za Mitaa, idara na wakala wa Serikali, pamoja na taasisi za kitaaluma na watafiti wanaojishughulisha na masuala ya maendeleo na uchumi.
Mkutano wa mwisho wa mwaka wa maafisa mipango ulifanyika mkoani Morogoro tarehe 12 Machi 2010 ambapo uliandaliwa na Wizara ya Fedha. Mada nne zilizowasilishwa na kujadiliwa zilikuwa ni;
i. Wajibu wa wataalamu wamipango katika Maendeleo ya Uchumi: Mipango ya Kiuchumi, Utekelezaji na Uandaaji wa Taarifa;
ii. Soko la Pamoja la Afrika ya Mashariki;
iii. Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa Wafanyabiashara Wadogo na Wakati; na
iv. Ufanisi wa Uwekezaji kutoka nje katika Uchumi wa Tanzania
No comments:
Post a Comment