Sunday, 14 September 2014

MBAGALA WAMUOMBA KIKWETE

Zaidi ya waathirika 1,300 wa mabomu yaliyolipuka Mbagala na kusababisha vifo na uharibifu wa mali, wamemwomba Rais Jakaya Kikwete kuwasaidia ili wapate fidia ya mali zao kama alivyokuwa ameahidi alipowatembelea.

Mabomu hayo yalilipuka Aprili 29, 2009 katika Kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) KJ 671 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 20, huku mamia wakijeruhiwa na familia nyingi kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomoka kabisa.
Wakizungumza jana, walisema kuwa Serikali inapiga ‘danadana’ suala lao, wakati idadi yao inazidi kupungua, kwani tangu wameanza kufuatilia fidia hiyo, wenzao 17 wameshafariki dunia kabla ya kupata haki zao.
Mwenyekiti wa waathirika hao, Steven Gimonge alisema kuwa ingawa Rais Kikwete alipowatembelea baada ya tukio hilo aliwaambia kuwa watalipwa hata vijiko vilivyo haribika, baadhi yao wamelipwa hundi za Sh1,400 na Sh1,950.
Kutokana na malipo hayo kuwa kidogo, walimwandikia barua Rais Kikwete Machi mwaka huu wakitaka waandamane, lakini walizuiwa kwa madai kuwa suala lao linashughulikiwa.
“Tunaambiwa tu subiri subiri; subiri hii mpaka lini hata kama alikuwa mtu amebeba mimba angekuwa ameshazaa na mtoto ameanza shule…au walitutoa kafara?
“Rais Kikwete agundue kwamba kumbe kuna wanaMbagala niliowaahidi watalipwa hadi kijiko kumbe hawajalipwa kabisa,” alisema Gimonge.
Aliongeza kuwa baada ya mlipuko wa mabomu, Serikali na wadau wengine walipeleka fedha, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida haijulikani ni nani aliyepewa.
“Vitu vililetwa yakajaa madarasa mawili, saruji tani 2,500, mabati tani 2,500 na magodoro, hatukupewa hata mtu mmoja.
“Kama tunavyosema sisi ni yaya (msichana wa kazi) amekula akifikiria kwamba mtoto amekula, kumbe sivyo. Tunamwomba Rais na wapenda amani duniani watuunge mkono, hata kama hela zilitolewa na wafadhili sisi hatukupewa, walikula wenyewe,” alisema.
Akishuhudia namna mabomu hayo yalivyomwathiri kiafya, Mwenyekiti huyo alisema kuwa alipata kifua kikuu mara mbili na kwamba hivi sasa anatibiwa saratani ya kibofu.
Kuhusu malipo
Wakati wa kupokea hundi ilibainika kuwa kuna tofauti kubwa ya malipo wakati athari na thamani ya nyumba inaonekana kuwa sawa.
Akitoa mfano alisema kuwa, “Utakuta mtu maafa namba 18 amepata Sh40 milioni wakati namba moja amepata Sh20, 000 au Sh2,000. Sisi kama waathirika tunashindwa kujua nini walikuwa wakizingatia katika kulipa malipo hayo.”
Aliongeza kuwa, “Ndani ya hundi zetu za Sh2,000 utakuta kuna vitu ambavyo vimejificha. Inaonekana kuwa watu ‘waliscan’ zile hundi zetu na kuandika sifuri nyingine, wakaziondoa na kuandika hundi nyingine tofauti.”

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!