Wednesday, 3 September 2014

M AFUNGU YA UKIMWI YANAZIDI KUSHUKA, MAAMBUKIZI MAPYA YASHIKA KASI


Wakati watu watatu walipothibitika kuwa na maambukizi ya Ukimwi mwaka 1983, hakuna ambaye angeweza kutabiri kile ambacho kingeweza kutokea miaka michache baadaye.

Kubainika na kuthibitika kwa watu hao, kulifuatiwa na mfululizo wa vifo na maambukizi mapya lukuki kwani hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 1999 watu wengine 118,713 walikuwa tayari wahanga wa ugonjwa huo.
Mwaka 1999 ikiwa ni zaidi ya miaka 16 toka kubainika kwa ugonjwa huo Serikali kupitia Rais Benjamin Mkapa ilitangaza kuwa ugonjwa huo ni janga la Taifa na Mkoa wa Kagera ukapewa uangalizi wa kipekee.
Mkoa huo ukawa unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya ugonjwa huo na kuacha maafa mabaya katika historia ya maradhi nchini kutokana na vifo na idadi kubwa ya yatima ambao walipoteza wazazi wao.
Wadau hao ambao walijikita zaidi katika utoaji wa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo ili kupunguza vifo na maambukizi, misaada kwa yatima na kutokana na kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo kampeni mbalimbali zikaanza nchi nzima.
Ikiwa ni miaka 10 sasa toka wahisani wajitose katika mapambano hayo na mingine 31 toka ugonjwa huo kubainika nchini, hivi sasa zaidi ya watu milioni 2.6 wanaishi na Virusi vya Ukimwi ambao umeishaua mamilioni ya watu hadi.
Pia watu 663,911 ikiwa ni pamoja na watoto 50,980 chini ya miaka 14 wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) na jitihada zinafanyika za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donald Mbando anawataka wahisani kubadili mwelekeo katika mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kuwawezesha wanawake kiuchumi ili kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa huo.
Anabainisha kuwa ndani ya kipindi hicho kumekuwa na mafanikio makubwa ingawa sasa kuna changamoto mpya ambayo ni umaskini kwa wanawake kwani ongezeko la maambukizi mapya ni makubwa.
Dk Mbando anasema kulingana na takwimu za karibuni, asilimia 6.2 ya wanawake wameambukizwa Ukimwi ukilinganisha na asilimia 3.8 ya wanaume hali ambayo inaonyesha wazi kuwa kuna jitihada mpya zinahitajika kukabili hali hiyo.
Anasema kuwa maambukizi ya Ukimwi ni tishio na ingawa takwimu za Kitaifa zinatajwa kuwa kiwango cha maambukizi ni asilimia 5.1, lakini hali ni tofauti katika baadhi ya mikoa.
Takwimu
“Hizo ni takwimu za kitaifa lakini kuna mikoa kiwango cha maambukizi ni kikubwa zaidi ya hicho cha kitaifa,” anasema na kuitaja mikoa hiyo na asilimia zake katika mabano kuwa ni Njombe (14.8), Iringa (9.1) na Mbeya (9).
Anasema kuwa kinachoonekana ni wazi kuwa kunahitajika kazi ya ziada kuzuia maambukizi mapya, unyanyapaa na kuwawezesha wanawake kupambana na janga hilo la kitaifa.
Dk Mbando anasema katika kipindi cha miaka 10 kumekuwa na mafanikio makubwa lakini hata hivyo safari bado ndefu kwani kasi ya maambukizi mapya miongoni mwa wanandoa na vijana inatisha.
Anasema maambukizi yamekuwa yakibadilika kwa namna nyingi na mikoa ambayo awali haikutarajiwa sasa kasi yake inatisha hali ambayo inafanya jitihada mpya kuelekezwa huko.
Mbando anasema chanjo hiyo ipo ya tatu kitabibu ambayo ni majaribio kwa binadamu na kuna watu ambao tayari wanafanyiwa majaribio katika mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya na Dar es Salaam.
Mratibu wa miradi katika shirika la Catholic Relief Services (CRS), Dk Selela Masuka anasema pamoja na changamoto na mafanikio ambayo yamefikiwa, bado kuna changamoto nyingi.
Anazitaja kuwa ni pamoja na uhaba wa fedha katika utekelezaji mbalimbali wa Ukimwi nchini hali ambayo inatokana na wahisani kupunguza mafungu ya fedha katika mapambano hayo.
Hali hiyo anasema imesababisha misaada kwa yatima kupungua na huduma za msingi kukosekana jambo ambalo linapaswa kutazamwa kwa namna ya pekee ili kusaidia kupunguza kasi ya maambukizi.
Tume ya Kuthibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) katika taarifa yake ya karibuni kwa vyombo vya habari, inalalamikia ukosefu wa fedha kutokana na wahisani kukatisha kuipa msaada.
Kulingana na ripoti hiyo, fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ambayo ipo chini ya tume hiyo ni wastani wa Sh1 trilioni lakini kiasi ambacho wanaambulia ni Sh500 milioni.
Taarifa zaidi zinabainisha kuwa wahisani wameacha kusaidia masuala ya Ukimwi kutokana na kuanzishwa kwa mifuko mbalimbali na kwa sasa wamejikita zaidi katika masuala mengine ya afya kuliko Ukimwi.
Alisema kwa sasa wana wafadhili wawili kati ya hao ambao wamekuwa wakiwapatia msaada ambao ni mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Ukimwi (PEPFAR).
Pamoja na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (GFATM) na kukabili upungufu huo wa rasilimali fedha, Serikali imechangia Sh300 bilioni kuwasaidia watu ambao wanaishi na Virusi vya Ukimwi badala ya kutegemea wahisani.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!