Taarifa kutoka idara ya ulinzi ya Marekani Pentagon zinasema kuwa mmoja wa wanzilishi wa kundi la Al Shabaab Ahmed Godane ameuawa.
Marekani imesema kuwa kuuawa kwa Godane ni hatua kubwa sana katika harakati dhidi ya wapiganaji hao wamekuwa msumari mkali kwa mataifa ya kanda ya Afrika Mashariki na hata kwa serikali ya Somalia yenyewe.
Kwa Mujibu wa Admiral Kirby, kuuawa kwa Godane ni pigo kubwa zaidi kwa kundi hilo la Al shabaab na itasaidia kukabiliana na ugaidi unaofanywa na kundi hilo eneo la Afrika Mashariki.Katibu wa Pentagon Nchini Rear Admiral John Kirby ametangaza kuwa Ahmed Godane ameuawa katika oparesheni iliyofanywa nchini Somalia Jumatatu wiki hii.
Marekani imekuwa ikishirikiana na washirika wake wakuu kukabili wapiganaji hao wa AL shabaab ambapo katika miaka ya hivi karibuni wamezidisha mashambulio sio tu nchini Somalia bali hadi nchi jirani.
Wiki iliyopita Kikosi cha kulinda amani chini ya mwavuli wa Muungano wa Afrika AMISOM kikishirikiana na majeshi ya serikali ya Somalia kilianzisha oparesheni kali kuwasaka wapiganaji hao wa AL shabaab. Na kufikia mwanzoni mwa wiki hii Marekani ikajiunga katika oparesheni hiyo ambapo walishambulia msafara ambao Ahmed Godane alishukiwa kuwa ndani.
Walioshuhudia waliambia BBC kuwa muda mfupi baada ya msafara huo kushambuliwa, ndege za kivita za helikopta zinazoaminiwa kuwa za Marekani zilishuka na kubeba maiti zote zilizo kuwepo. Kwa hiyo kwa muda hakukuwa na thibitisho lolote iwapo Godane mwenyewe aliuawa au la.
Upande wa AL shabaab nao walianza kukusanya watu katika kijiji karibu na eneo hilo la Shebeele ambako shambulio lilifanywa na kuwaua au kuwateka wengijne ambao hadi sasa hawajulikani waliko.
AL shabaab hawakuzungumzia iwapo Godane alikuwa miongoni mwa waliouawa.
Leo asubuhi kulikuwa na picha zilizo sambazwa katika mtandao ambazo hazikuthibitishwa zilizodai kuwa ni Ahmed Godane bado alikuwa hai.
Al shabaab hawajasema lolote baada ya tangazo la Pentagon kuthibitisha kifo cha Godane
No comments:
Post a Comment