KENYA imeadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutokea kwa tukio la kutekwa na kushambuliwa na kundi linalodhaniwa kuwa la ugaidi katika maduka ya Westgate na kusababisha vifo vya watu takribani 67.
Katika kumbukumbu hiyo, kutakuwa na tendo la kuwasha mishumaa kwa ajili ya kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha yao katika tukio hilo kubwa nchini Kenya.
Tukio la kutekwa na kushambuliwa kwa maduka hayo lilichukua takribani siku nne, huku kamera za CCTV zikionesha wateja waliokuwamo ndani ya maduka hayo wakihaha kwa hofu na kujaribu kujiokoa dhidi ya watu waliokuwa na silaha walioteka maduka hayo.
Kundi la kigaidi la Al-Shabaab kutoka nchini Somalia lilijitangaza kuhusika na shambulio hilo na kudai kuwa limefanya hivyo baada ya majeshi ya Kenya kupelekwa katika operesheni nchini Somalia.
Ndugu na jamaa wa marehemu waliopoteza maisha yao katika tukio hilo, waliweka mashahada ya maua katika bustani ya miti 67 iliyopandwa maalumu baada ya kutokea kwa shambulio hilo. Na baada ya hapo sala mbalimbali zitaendeshwa kwa ajili ya kuziombea roho za marehemu.
“Tunatarajia ndugu na jamaa wa marehemu watajitokeza na kuwa sehemu ya kumbukumbu hii,” alisema Mratibu wa maandalizi ya kumbukumbu hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mmoja wa wavamizi katika maduka hayo, alioneshwa katika video za CCTV, akiwinda wateja waliokuwemo ndani ya duka hilo na nyingine zikionesha namna watu wanavyouawa huku sehemu kubwa ya maduka hayo ikiharibiwa vibaya.
No comments:
Post a Comment