Tuesday 2 September 2014

BODA BODA NI JANGA LA TAIFA- MWENDESHA BODA BODA AFARIKI

MWENDESHA pikipiki (bodaboda), Moshi Ramadhani (27) amekufa papo hapo huku abiria aliyekuwa amembeba ambaye ni Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, amesagika mguu na kuvunjika mkono, baada ya kugongwa na basi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philpo Kilangi, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema ni ya jana saa 12 asubuhi, katika barabara kuu ya Musoma-Mwanza, eneo la Bunda mjini.
Kilangi alisema kuwa watu hao waliokuwa wamepakiana kwenye pikipiki hiyo waligongwa na basi mali ya Kampuni ya Bunda Express, lililokuwa linatoka Mara kuelekea Dodoma. Alisema Ramadhani ni mkazi wa Kijiji cha Kabasa, wilayani Bunda.
Alimtaja Ofisa Utamaduni aliyejeruhiwa vibaya kuwa ni Juma Sindano (59). Kamanda alisema kuwa majeruhi huyo amelazwa Katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda, na alifikishwa hapo akiwa amesagika kabisa mguu na kuongeza kuwa madaktari walilazimika kumkata mguu huo kutokana na kujeruhiwa vibaya.
Alisema kuwa dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T 234 DZK, aliyetambuliwa kwa jina la Yunus Lutungo (36), mkazi wa Nyakato jijini Mwanza, anashikiliwa na Polisi na atafikishwa Mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Daktari katika chumba cha upasuaji hospitalini hapo, Dk Armstrong Mpemba, alisema kuwa walilazimika kuukata mguu huo wa kulia na kuuondoa kabisa kutokana na kuwa katika hali mbaya na kwamba wasingeweza kuunga.
“Mguu huo ulikuwa umesagika vibaya, hivyo tuliamua kuuondoa kwani isingewezekana kuunganisha, kutokana na jinsi ulivyokuwa,” alisema Dk Mpemba.
Dk Mpemba alisema kuwa mkono uliojeruhiwa ni wa kulia na kwamba wanaendelea kuunganisha na kuongeza kuwa sasa hivi anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo kimesababishwa na mwendesha pikipiki huyo kuingia ghafla barabarani na kukutana na basi hilo, lililokuwa kwenye mwendo kasi.
Wakati huohuo Sophia Mwambwe anaripoti kuwa, kijana aliyekuwa anaishi Dar es Salaam amekufa na wengine wawili kujeruhiwa katika matukio mawili yaliyotokea jijini humo.
Katika tukio la kwanza muendesha pikipiki aliyefahamika kwa jina la Godlisten Kimambo (40) mkazi wa Kiwalani akitokea Ubungo kwenda Tabata aligongana na UDA namba T 766 CNS katika barabara ya Mandela, juzi saa 3 usiku eneo la Mwananchi na kufa.
Alikuwa na pikipiki namba T 808 AYK, Honda. Kamanda wa Polisi Kinondoni, Camillius Wambura alisema UDA ilikuwa ikiendeshwa na Magina Ally na Kimambo alikufa papo hapo.
Alisema mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio la pili, Polisi wa Kituo cha Msimbazi, Nyangongo Mtiga akiendesha gari aina ya Toyota Avencis yenye namba Z 486 CN alimgonga mwendesha pikipiki, Thomas Joseph katika barabara ya Nyerere eneo la Mtava.
Kamanda wa Polisi Ilala, Mary Nzuki alisema gari hilo lilikuwa likitokea upande wa Tazara kwenda mjini.
Alisema gari lilihama njia ghafla, likaserereka na kugonga mti na kusababisha ajali hiyo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!