Wednesday 17 September 2014

BEI YA UMEME KUSHUKA


SERIKALI imesema inatarajia kuondoa mitambo yote inayotumia mafuta katika kuzalisha umeme ifikapo Januari mwakani. Hali hiyo itaokoa Sh trilioni 1.6 kwa mwaka, lakini pia kuwapa Watanzania umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.


Mitambo hiyo itaondolewa kwenye gridi ya taifa huku mitambo mingine inayotumia mafuta, ikibadilishwa na kutumia gesi, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi unaoendelea pamoja na mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi wa Kinyerezi I, Dar es Salaam, ifikapo Januari hadi Machi mwakani.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi katika ziara ya mabalozi na wafadhili nchini ya kutembelea na kuona maendeleo ya ujenzi wa bomba hilo la gesi na mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi wa Kinyerezi I.
Alisema tayari wameanza kuchukua hatua za kuondoa baadhi ya mitambo inayozalisha umeme kwa kutumia mafuta yenye megawati takribani 150, ambayo ni mtambo wa umeme wa Arusha wenye megawati 50 na Dodoma megawati 100.
“Baada ya kukamilisha ujenzi wa bomba hili la gesi tutapunguza mitambo hii inayotumia mafuta, lakini pia tutatumia mitambo yetu iliyopo inayotumia gesi, lakini kwa kiasi kidogo kutokana na uhafifu wa gesi hiyo kwa sasa, na kutumia gesi inayotoka Mtwara hadi Dar es Salaam, hili tukilifanikisha tutakuwa na ziada ya megawati 300 ya umeme,” alisema Maswi.
Alisema kwa sasa kuna mtambo wa kuzalishia umeme kwa kutumia gesi wa Ubungo, unaozalisha megawati 105, lakini unazalisha megawati 30 na mtambo wa Ubungo I wenye uwezo wa kuzalisha megawati 100, lakini unazalisha megawati 68 tu, kutokana na ufinyu wa gesi inayotumika sasa kutoka Mnazi Bay.
“Gesi ni muhimu ikianza kupatikana Januari ili mitambo hii yote tuiunganishe na gesi hii ya Mtwara pamoja na ule mtambo wa Symbion unaozalisha megawati 112, ambao kwa sasa unazalisha umeme kwa kutumia mafuta ndege,” alisema.
Alisema kukamilika kwa bomba hilo na kuanza kuzalishwa kwa umeme kwa kutumia gesi, kutawapunguzia wananchi gharama kubwa zilizopo sasa za umeme, lakini pia kuwapatia umeme wa uhakika, ambapo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) nalo litajiendesha kwa faida.
Aidha, Maswi aliwahakikishia wakandarasi wanaojenga mtambo huo wa kampuni ya Jacobsen Elektro, kuwa kiasi cha fedha kilichobakia, kitakamilishwa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha kwa kuwa tayari kipo kwenye bajeti.
Awali, akitoa maelezo kwa ujumbe huo, Meneja Mradi wa Ujenzi wa Mtambo wa Kuzalisha Umeme wa Kinyerezi I, Simon Jilima, alisema ujenzi wa mtambo huo unaendelea vizuri na kwa sasa umefikia asilimia 75 ili uweze kukamilika.
Alisema mradi huo, utakamilika rasmi Januari mwakani na kufanyiwa majaribio ya mitambo, ambapo Machi mwaka huo utakabidhiwa kwa Serikali tayari kwa kuingiza megawati 150, zitakazolishwa kwenye gridi ya taifa ya umeme.
“Mtambo huu tunaujenga kwa kasi na tunakwenda vizuri na wakati, tumebakisha vitu vidogo hasa vifaa vinavyoendelea kuingia nchini, tutakapoanza kuzalisha tutatumia gesi ya Mtwara, lakini pia kuna matangi mawili ya mafuta ya ndege na mafuta ya taa kwa ajili ya kuzalishia umeme pindi gesi itakapopatwa na dharura.
Alisema mradi huo wa Kinyerezi, umegharimu dola za Marekani bilioni 1.83 (Sh trilioni 3) na hadi sasa Serikali kupitia Tanesco imelipa dola za Marekani milioni 128 (Sh bilioni 211).
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba, alisema ujenzi wa bomba hilo kwa sasa umekaribia asilimia 98 na ni kilometa tano pekee, ndio zilizobakia kati ya kilometa 542 za bomba hilo zinazotandikwa.
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Uganda na Burundi, Philippe Dongier, alisema maendeleo ya mradi huo yanaridhisha na utakapokamilika kilio cha muda mrefu cha watanzania cha upungufu wa umeme, kitapatiwa ufumbuzi.

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!