Thursday, 28 August 2014

WIZARA YA AFYA ZANZIBAR YAKABIDHI VIFAA VYA KUCHUNGUZA EBOLA



Wizara ya Afya Zanzibar imekabidhi kifaa cha THERMAL SCANNER kwa ajili ya kuchunguza Wagonjwa wa EBOLA watakao ingia nchini kutoka mataifa mengine.

Kifaa hicho kilichowekwa katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume kitatumika kwa ajili ya kuwachunguza zaidi Wageni ambao watatoka katika nchi zilizoathiriwa na Ugonjwa wa Ebola.

Akikabidhi kifaa hicho Mkuu wa kitengo cha kufuatilia mwenendo wa Maradhi Zanzibar Dkt Salma Masauni amesema THEMO SKAN kitasaidia katika kuwabaini watu ambao wameathirika au kuwa na dalili za Ungojwa wa Ebola na kuchukuliwa hatua zaidi.

Dkt Salma amesema iwapo mgonjwa atabainika hatua zaidi zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kupelekwa katika kituo cha Afya cha Chumbuni ambacho kimetayarishwa kwa ajili hiyo.


Aidha Dkt Salma amefahamisha kuwa Kituo cha Afya cha Chumbuni kimetengwa kama eneo litakalotumika kwa ajili ya Matibabu kwa mgonjwa atakayebainika kuambukizwa Ugonjwa wa Ebola nchini.

Amesema Wizara ya Afya katika kukabiliana na Ugonjwa huo wa kuambukiza imekuwa ikifanya Jitihada mbalimbali za kutoa elimu na njia mbali mbali za kinga kabla ya Zanzibar kuathirika na Ebola.

Amesema licha ya Vifaa hivyo vilivyotolewa Vifaa vingine vitakuja wiki inayokuja ili viendelee kutumika katika maeneo ya Bandarini na Viwanja vya ndege Unguja na Pemba

Dkt. Salma amesema Ugonjwa huo haujaingia nchini bali Serikali inajiandaa na juhudi zake za kukabiliana na Ugonjwa huo ili usiweze kuingia na kuathiri Zanzibar.


Kwa hisani ya Faki Mjaka Maelezo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!