Monday, 18 August 2014

VITAMBULISHO VYA URAIA HAVITATUMIKA KATIKA UPIGAJI KURA-NEC

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba



Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesisitiza kuwa vitambulisho vya taifa vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), havitatumika kupiga kura katika uchaguzi mkuu, isipokuwa kadi zitakazotolewa na tume hiyo.



Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba alifafanua jana jijini Dar es Salaam kwamba ni makosa kudhani kuwa vitambulisho vinavyotolewa na Nida, vinaweza kutumika kupiga kura.
“Haiwezekani kabisa…tunaomba watu waelewe kuwa kadi za kupiga kura na vitambulisho vya uraia ni vitu viwili tofauti. Vitambulisho vya taifa siyo mbadala wa kadi za kupiga kura,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kwa hali ilivyo utoaji wa vitambulisho vya taifa kwa nchi nzima, utachukua muda mrefu na kwamba hata baada ya uchaguzi ulioagizwa kisheria kupita, watu wengi watakuwa hawajapata vitambulisho hivyo.
Mkurugenzi alitoa ufafanuzi huo, kutokana na kile alichosema ni kutokana na kuwepo taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba mtu asiye na kadi ya kupiga kura, anaweza kutumia kitambulisho cha uraia kupiga kura.
Alisema wakati uandikishaji wa NEC unafanyika kwa muda maalum ili kuwahi upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu, uandikishaji wa Nida hauna muda maalumu.
“NEC ina mchakato mfupi wa ukusanyaji wa taarifa za watu wanaoandikishwa na kadi za mpiga kura zinatolewa papo hapo kituoni baada ya ujazaji wa fomu,” alisema.
Kwa upande wa Nida, mchakato wa ukusanyaji wa taarifa una utaratibu mrefu kutokana na wahusika wa zoezi hilo kuwa wengi.
Akielezea zaidi alisema namba ya kadi inayotolewa na tume ya taifa ya uchaguzi ni ya kipekee kwa mtu anayeandikishwa.
Nida inaweza kutoa namba zaidi ya moja endapo itabidi kutoa kitambulisho kingine kwa mtu huyo huyo, kutokana na kitambulisho cha awali kupotea au kuharibika.
Mallaba alisema hata kama vitambulisho vya uraia vingekuwa tayari, bado tume ingetakiwa kuandaa daftari kwa kuwa vitambulisho vya uraia huwa haviainishi mtu ni mpiga kura wa eneo gani.
Alifafanua kuwa kama wananchi wote wangekuwa na vitambulisho vya taifa, kitu ambacho kingefanyika ni kwa tume kununua kifaa kinachoweza kusoma kitambulisho na kupata taarifa za mhusika na kumpangia mhusika sehemu yake ya kupigia kura.
Alisema hakuna nchi katika bara la Afrika, inayotumia kitambulisho cha taifa moja kwa moja katika kupiga kura, isipokuwa hutumika kurahisisha utaratibu wa kuandaa daftari la kudumu la wapiga kura.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema uandikishaji wa vitambulisho vya taifa kwa upande mmoja na vitambulisho vya wapiga kura kwa upande mwingine ni shughuli tofauti, lakini zinazohusiana kwa karibu na pia zinazohusu wananchi.

CHANZO: HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!