Sunday, 17 August 2014
TUSIPOKEMEA JINAMIZI LA AJALI LITATUMALIZA!
JINAMIZI la ajali limeendelea kutawala katika barabara za nchi hii na kusababisha watu kupoteza maisha na wengine kubakia na ulemavu katika viungo vyao vya mwili.
Kila siku ni matukio ya ajali pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Kikosi cha Usalama Barabarani kuhakikisha Watanzania wanasafiri salama.
Hata hivyo juhudi hizo zimekuwa zikirudishwa nyuma na baadhi ya madereva wazembe ambao mimi nawaita ni waendesha magari kwa sababu dereva makini hawezi kufanya uzembe na kusababisha ajali ambazo zingeweza kuepukika na kuokoa maisha ya watumiaji wa vyombo vya usafiri.
Wiki hii inayokwisha kumekuwa na taarifa za ajali ikiwemo ajali iliyoua watu 18 na kujeruhi 56 mkoani Dodoma waliokuwa katika basi la Morobest.
Kilichonishangaza na kunishtua ni taarifa ya polisi mkoani Dodoma ambayo ilisema ushahidi uliokusanywa, umebainisha kwamba dereva wa Morobest Saidi Lusogo (ambaye alikufa kwenye ajali hiyo) alisema mwanafunzi wake aliyekuwa dereva wa Al Saedy hawezi kufika Morogoro kabla yake hivyo aliamua kumpita.
Hivi kweli dereva makini anaweza kusahau amebeba abiria na kuanza kushindana na dereva mwingine, eti kwa sababu tu alimfundisha kuendesha gari, hawa ndio wale ninaosema ni waendesha magari na si madereva.
Ajali nyingi zinazotokea kwa kweli ni uzembe unaofanywa na waendesha magari ambao hawajui ama hawataki kuzingatia Sheria za barabarani na matokeo yake wameendelea kusababishia Watanzania vifo na ulemavu bila huruma.
Unapokuwa barabarani unaweza kuona mambo mengi ya ajabu yakitendeka mpaka unashangaa hivi watu wanaofanya hivyo wanaamini kuna uhai mwingine au wana matatizo ya kufikiri?
Dereva anasahau amebeba watu wengi, wana familia zao, wana shughuli zao lakini kwa sababu ya kutokujali na kufikiri unasahau na kudhani umebeba mizigo badala ya binadamu na yanapotokea ya kutokea hata kama wewe dereva utakimbia au kupoteza maisha tayari utakuwa umeharibu maisha ya wengi uliowabeba waliokuwa na matarajio ya kufika salama kule wanakoelekea.
Lakini pia abiria nao wanakuwa na matatizo, ama ni woga, kutokujali au kutofahamu kuwa wana haki ya kumdai dereva kuendesha kwa umakini.
Hii tabia ya abiria kukaa kimya na kuacha kumuonya dereva anapoendesha gari vibaya matokeo yake huwagharimu maisha yao.
Lazima abiria kupaza sauti na kukataa kukaa kimya pale dereva anapoleta mchezo barabarani, gari ni chombo cha moto, kosa kidogo ni ajali, sasa kwa nini usilinde uhai wako mapema na kupaza sauti kwa kumuonya dereva au kutaarifu Polisi ili adhibitiwe.
Bora abiria muonekane wakali na mna maneno kuliko kukaa kimya halafu ikitokea ajali, ndio mnaanza kusema kuwa dereva alikuwa anaendesha kwa mwendo kasi wakati mlikuwa na nafasi ya kumdhibiti mapema.
Umelipa fedha yako ukiamini utasafirishwa na kufika salama, kwa hiyo unapoona tofauti ya uendeshaji unayo haki ya kuhoji au kumuonya dereva na kama atakaidi toa taarifa polisi, hizi tabia za woga na kutojiamini ndio hugharimu maisha ya watu.
Kama dereva mzembe njiani kuna askari wa Usalama Barabarani semeni, pazeni sauti kuseme tatizo la uendeshaji mbovu wa dereva, kama abiria mtakuwa wakali huenda ikasaidia kuwafanya madereva wazembe kuogopa na kuwa makini barabarani.
Wakati wa Watanzania kupaza sauti na kukataa kukatishwa maisha au kusababishiwa ulemavu na madereva wazembe wasiojali Sheria na Taratibu barabarani. Naamini kama Watanzania tutaungana kukataa na kukemea ajali hizi zitakoma kama sio kwisha kabisa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Alhaji Chambo16:19
1
duu ajal mbaya kwel yn
Post a Comment