Sunday, 17 August 2014

SERIKALI- MSIHOFU HAKUNA EBOLA NCHINI



SERIKALI imewataka Watanzania kutokuwa na hofu ya ugonjwa wa ebola kwani wamejipanga ipasavyo na hakuna mgonjwa aliyethibitika kuwa na ugonjwa huo. Imesisitiza hivyo baada ya kuwapo na taarifa zisizo rasmi kwamba ugonjwa huo umeshaingia nchini.



Kauli hiyo ya Serikali ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Shaaban Mwinjaka wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Alisema kumekuwa na baadhi ya vyombo vya habari vinavyotangaza kuwepo kwa wagonjwa wa ebola nchini lakini habari hizo si za kweli na zinatolewa na watu bila kufanya uchunguzi.
“Suala la ebola sio la kuongelea kwa mzaha, ni vyema watu wafuatilie na kujua ukweli ndipo taarifa zitolewe kwani ugonjwa huu unatisha na hauna dawa,” alisema Mwinjaka.
Alisema Serikali imejipanga vizuri karibu kila eneo, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege ambako wataalamu zaidi ya 17,000 wamesambazwa ili kuhakikisha hakuna mgonjwa yeyote atakayeingia nchini bila kuchunguzwa ugonjwa huo.
Aliongeza kuwa watu wawili waliokuwa wanahisiwa kuwa na ugonjwa huo juzi, baada ya kuonekana na dalili za ugonjwa huo ndipo watu walianza kusambaza habari za kuwepo kwa ebola nchini.
Alisema mgonjwa wa kwanza aliyedhaniwa kuwa na ugonjwa huo juzi, alikuwa akisafiri kwenda Mbeya kwa ndege ya Fastjet akiwa katika sehemu ya kupumzikia abiria alianza kutokwa na damu puani na watu walihofia kuwa ni ebola, lakini baada ya uchunguzi ilibainika kuwa alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo.
Mgonjwa mwingine ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika ya jijini Dar es Salaam, alikuja likizo kwa baba yake ambaye anaishi Msasani alidhaniwa kuwa na ebola baada ya kuonekana ana homa kali, lakini baada ya uchunguzi alibainika kuwa na malaria, hivyo alitibiwa na kuondoka.
Mkurugenzi Msaidizi wa Maafa katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elias Kwesi alisema mpaka sasa hakuna mgonjwa wa ebola nchini, bali watu wanaongozwa na hisia hasa mtu anapoonekana na dalili mojawapo.
Alisema Serikali katika kudhibiti ugonjwa huu imepeleka dawa na vifaa vya kujikinga na ebola vimeshasambazwa nchi nzima, katika kila wilaya na kwamba, ingawa ugonjwa huo hauna tiba, wataoonekana kuwa na dalili za virusi vya ebola watatibiwa kutokana na dalili zake.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini, Suleiman Said Suleiman alisema viwanja vya ndege vipo tayari kukabiliana na ugonjwa huo na kwamba wana uzoefu wa kukabili magonjwa ya milipuko na pia wametoa elimu kwa wafanyakazi wote wamepewa elimu ya kumtambua mtu mwenye ebola, ndani na nje ya ndege.
Tayari katika viwanja vya ndege nchini kuna magari ya kubeba wagonjwa wa ebola ambayo ni maalumu kwa watu watakaobainika kuwa na ugonjwa huo na hayaingiliani na magari mengine ya wagonjwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!