SERIKALI imesema itajitahidi kutenga fedha katika bajeti yake, ambazo zitatumika kununua dawa za maradhi ya kisukari itakazozigawa bure kwa wagonjwa.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa pili wa ‘Pan African Diabetic Foot Study Group’ ambao ni wa siku tatu.
Alisema licha ya dawa za ugonjwa wa kisukari kuwa za gharama kubwa, upatikanaji wake nao umekuwa wa shida, hivyo kuwasumbua watu wenye maradhi hayo.
Dk. Rashid, alisema serikali itajitahidi kuweka kliniki za kisukari katika hospitali za wilaya ili wagonjwa wasihangaike kwenda mbali kupata huduma katika hospitali za mikoa.
“Serikali imeutambua ugonjwa wa kisukari kama moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ambayo wagonjwa wake wanapaswa kupewa dawa bure, nia ya dhati ipo ila fedha bado ndiyo linakuwa tatizo katika kutekeleza nia hiyo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Pan African Diabetic Foot Study Group, ambaye pia ni Mwenyekiti wa mradi wa miguu wa ‘Step by Step’, Dk. Zulfiqarali Abbas, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye mzigo mkubwa wa magonjwa ya kisukari.
“Tanzania ina mzigo mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza, sio tu kisukari bali na matatizo yanayoambatana na ugonjwa huu kama vile vidonda vya kisukari miguuni, ambalo ongezeko lake haliwezi kufumbiwa macho,” alisema Dk. Abbas
No comments:
Post a Comment