Saturday, 23 August 2014

PINDA AONGOZA MAMIA KUMUAGAJAJI MAKAME




MAMIA ya watu wakiwemo viongozi wa nyanja mbalimbali nchini, jana walijitokeza kuuaga mwili wa Jaji mstaafu, Lewis Makame kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, huku sifa za utendaji wakati wa utumishi wake zikitawala shughuli hiyo.



Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewataka watanzania na viongozi wote nchini kumuenzi Jaji Makame kwa kuendeleza utulivu na kufikiri kwa umakini kabla ya kufanya uamuzi, mambo aliyoyafanya wakati wa uhai wake.
Akitoa salamu za serikali za rambirambi, Waziri Pinda alisema nchi imeondokewa na mtu muhimu na mzalendo wa kweli.
Jaji Makame pia alikuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC), "Tumeondokewa na Mtanzania mzalendo wa kweli, alikuwa mtulivu na aliyefikiri kwa umakini kabla ya kufanya uamuzi”, alisema Pinda na kuongeza kuwa, ili kumuenzi, watanzania na viongozi wote wanapaswa kuendeleza mazuri aliyoyafanya kwa ajili ya ustawi wa nchi.
Naye Jaji Mkuu Othman Chande alisema Jaji Makame ametenda haki kwa taifa lake kwa miaka 47 ya utumishi wake na anastahili kuenziwa kama jaji kiongozi aliye mfano wa kutenda haki na kujali wadogo.
"Makame alikuwa mpenzi mkubwa wa sheria, aliifanya sehemu ya maisha yake na sio kazi, alikuwa na kipaji cha fani hiyo na hilo limeonekana kupitia hukumu alizoandika," alisema Jaji Chande. Alitoa mfano wa hukumu alizotoa ikiwemo ya mauaji iliyomkabili Doris Liundi aliyeua watoto wake na kusema hukumu hiyo ilivuta hisia za wengi hasa kwa jinsi ilivyoandikwa kwa umakini wa hali ya juu na ubora wa lugha. "Jaji hujenga au kubomoa sifa yake kutokana na kuendesha kwake kesi, kwa kweli alikuwa mmoja wa majaji wenye uwezo kuliko wote", alisema Chande. Aliongeza sifa kubwa nyingine ya Jaji Makame alikuwa kiongozi mwenye kujali watu wa rika zote na alikuwa miongoni mwa majaji wenye nidhamu ya juu na mtulivu wa kufanya uamuzi. Kwa upande wa salamu kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Abdulhakim Ameir Issa akisoma kwa huzuni salamu za rambirambi alimuelezea Makame kama kiongozi aliyesisitiza ushirikiano kutoka pande zote . Alisema ni pigo kubwa kwa taasisi zote za kidemokrasia nchini na hata nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)ambapo alikuwa msaada wa ushauri na uongozi wa masuala mbalimbali ya sheria na demokrasia. Akisoma salamu kutoka NEC, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema; “Msiba huu umetushitua sana, Makame alikuwa mwanzilishi wa tume hii na ndiye aliyekaa kwa muda mrefu awamu nne za uchaguzi alikuwepo ni miaka 18, kwa kweli alikuwa Kamusi inayotembea ya tume." Kwa upande wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alimwelezea Makame kuwa alikuwa kiongozi mwadilifu na aliyefanya kazi yake kwa umakini na uongozi bora, licha ya changamoto alizopitia. Shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Jaji mstaafu Makame ziliongozwa na Jaji mstaafu Padri Augustino Ramadhani na zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wastaafu, kama Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri wakuu wastaafu, Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba na Frederick Sumaye, majaji na mawaziri wastaafu. Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, dini, viongozi wa taasisi za serikali na binafsi pamoja na wananchi mbalimbali walijitokeza kwa wingi na kwa utulivu kuaga mwili wa Jaji Makame anayetarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Tongwe, Muheza mkoani Tanga. Makame alifariki dunia mwanzoni mwa wiki hii katika Hospitali ya Ami Trauma Centre, Dar es Salaam alikokuwa anatibiwa.

VIA-HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!