Yapo mambo ambayo ubongo wa binadamu unatakiwa kuyafanya kwa ufanisi ili mtu aonekane kuwa ana akili.
Mambo hayo ni kama vile kuwa na uwezo wa kujifunza na kuelewa kwa haraka, kutunza kumbukumbu na kuwa na uwezo wa kutumia tena taarifa zilizotunzwa katika ubongo ili kuzichanganua kulingana na hali halisi ya mazingira yanayomkabili.
Tunaweza kuutazama ubongo kama ilivyo kompyuta ilivyo na mfumo tata wa kuchakata taarifa ambayo utendaji wake hutegemea uwezo wa mtumiaji.
Hivyo ndivyo pia ilivyo akili ya binadamu. Akili hutegemea maumbile ya vitu vilivyomo ndani ya ubongo na mazingira ya nje,” anasema Dk Mohana Ali katika makala yake ya ‘The Biological-Environmental Hypothesis of Human Intelligence’ iliyochapishwa Julai, 2014 katika mtandao wa www.dana.org
Katika ubongo kuna nyaya zinazosafirisha taarifa kutoka seli moja kwenda seli nyingine ya ubongo. Nyaya hizi zimefunikwa na utando wa mafuta mafuta unaojulikana kama myelin.
Myelin kama ilivyo kwa vifuniko vya plastiki vinavyofunika waya wa umeme, huzuia mkondo wa taarifa katika seli za ubongo zisivuje na kwa maana hiyo huziwezesha kusafiri kwa haraka katika sehemu mbalimbali za ubongo.
Ubongo wenye myelin yenye ubora wa hali ya juu husaidia mtu kuwa na uwezo mkubwa wa kiakili.
Yapo mambo ambayo yanasaidia ubongo kuwa na afya nzuri na yanasaidia myelin kuwa katika hali nzuri. Ubongo unahitaji lishe bora na kuchangamshwa ili uweze kufanya kazi vizuri na kuwa na uwezo wa kiakili. Kwa maana hiyo akili zinalelewa na kukuzwa.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa lishe yenye kiasi cha kutosha cha wanga na sukari ni muhimu kwa ajili ya kuupatia ubongo nguvu.
Ulaji wa samaki pia husaidia ubongo kupata mafuta mafuta ambayo ni muhimu kwa ajili ya kukuza uwezo wa kiakili.
Kucheza, kufanya mazoezi na kuvuta hewa safi ya kutosha pia ni muhimu kwa ajili ya kuchangamsha akili na kuongeza uwezo wa ubongo kufanya kazi zake kwa ufanisi.
“Akili yako inahitaji mazoezi pia. Kama utaacha kujizoeza na kutumia uwezo wa akili na ujuzi wa kutatua matatizo, uwezo wa kufikiri na utambuzi wa mambo, utategemea vipi akili yako kuwa nyingi?” anauliza mtaalamu wa tiba ya tabia katika mji wa Florida nchini Marekani, Andrea Kuszewski.
Kadiri ubongo wa mtoto unavyochochewa kwa vichocheo na vichangamshi salama, ndivyo chembe nyingi zaidi za neva zinavyoanza kufanya kazi na kuunganishwa.
Ubongo wa mtoto hauchochewi na kukuzwa kupitia kufundishwa mambo, hesabu au lugha pekee. Wanasayansi wanasema kwamba ubongo wa mtoto unahitaji kuchochewa pia kihisia kwa upendo.
Tafiti nyingi za kisayansi zinaonyesha kwamba ubongo wa mtoto wadogo hauwezi kustawi vizuri iwapo hawakumbatiwi, hawaguswi, hawachochewi kihisia na wale wasioshiriki katika kucheza.
Dk Samwel Shita wa gazeti hili, anasema kwamba kucheza kunachangia kukuza uwezo wa akili.
“Miongoni mwa faida za kiafya za kucheza kwa watoto ni kupata afya bora ya ubongo, kujijengea ujuzi, kukuza ufahamu…kumjengea uwezo wa ufanyaji uamuzi na kukuza kipaji,” anasema Dk Shita.
Mtaalamu wa masuala ya saikolojia ya watoto wa hapa nchini, Denis Munga aliwahi kukaririwa akizungumzia watoto wanaocheza na kuonyesha utundu mwingi kuwa ni wenye akili nyingi.
Munga anaongeza kusema: “Ili kufahamu kama akili za mtoto zinafanya kazi vizuri, mzazi anatakiwa achunguze kama mtoto ana tabia ya kushughulishwa na vitu vilivyo karibu yake.”
Mwanasaikolojia na daktari bingwa wa watoto na upasuaji wa ubongo, Benjamin Carson wa Marekani anasema: “Hakuna mtu mwenye akili ndogo. Ikiwa una ubongo wa kawaida na wenye afya njema, wewe ni mtu mwenye uwezo mzuri kiakili.”
Dk Carson anachukua mfano wa yeye mwenyewe akisema: “Mimi nilikuwa mwanafunzi mwenye uwezo mdogo sana wa kiakili darasani. Nilikuwa mwanafunzi wa mwisho darasani kiasi kwamba wanafunzi wenzangu na walimu wangu walikuwa wananiita zoba. Jambo lililonifanya kuchukia sana na kuwa mtu mwenye vurugu.”
Anaendelea kusimulia kuwa mama yake kuona hivyo aliamua kumsaidia kwa kumtia moyo kwa upendo na upole na kumpangia ratiba maalumu ya kujisomea kila siku.
Anasema baada ya muda alianza kufanya vizuri darasani. Mwaka mmoja baadaye alishika namba ya kwanza darasani. “Ni katika kipindi hicho ndipo nilipotambua sikuwa mbumbumbu,” anasema.
Mwaka 1987, Dk Carson aliushangaza ulimwengu kwa kuweka historia ya kipekee katika fani ya tiba ya upasuaji kutokana na kufanikisha upasuaji wa pacha walioungana vichwa ambao ulichukua saa 22
Thomas Alva Edison, mgunduzi wa balbu za umeme aliwahi kusema kuwa akili nyingi kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya kufanya bidii katika kufikiri na kufanya kazi ili mambo mazuri uliyokusudia yatokee.
Edison aliyasema hayo baada ya kushindwa mara nyingi katika majaribio ya ugunduzi wake lakini hakukata tamaa na hatimaye alifanikiwa.
Katika kipindi cha utoto wake, walimu wake walimuona kama mtoto mwenye uwezo mdogo wa kiakili lakini hilo halikumkatisha tamaa.
Naye, Walter Isaacson, mwandishi aliyeandika habari za maisha ya watu wenye akili nyingi kama Steve Jobs mgunduzi wa iPod, Albert Einstein na Benjamin Franklin anasema watu hawa wote walikuwa na tabia zinazofanana kama vile kuwa na tamaa na malengo ya kufanya vitu tofauti na kuwa na maono au ndoto walizotaka zitimie.
Isaacson anaongeza kusema kuwa watu hao pia walijua namna ya kutumia akili za watu wengine ili kufanya mambo yatokee.
Waliamini kuwa akili nyingi ni uwezo wa kutumia akili za watu wengine ili kupanua uwezo wa kufikiri na kubuni.
Walitoa pia changamoto kwa fikra za wengine lakini waliamini kuwa ubongo wao una uwezo wa kutatua changamoto zao na binadamu wengine.
Dr Alfred Barrious mtaalamu bingwa wa saikolojia ambaye pia ni mwandishi wa kitabu cha Towards Greater Freedom and Happiness cha mwaka 1978, anasema “ watu wengi hufanya makosa kufikiri kuwa watu wenye akili nyingi wamerithi uwezo wote wa kiakili ila ukweli ni kwamba wamewezeshwa pia na mazingira yao kuwa na akili”
Naye Luciano M na wenzake katika utafiti wao wa mwaka 2004 uliochapishwa katika jarida la ‘Behavior Genetics’ toleo la 34, anabainisha kuwa uwezo wa akili kufanya kazi haraka na kubuni mambo unatokana na urithi wa vinasaba pamoja na kukuzwa na mazingira.
Ripoti ya Chama cha Wataalamu wa Saikolojia nchini Marekani kilitoa ripoti yake Agosti 1995, kikisema kwamba watu hutofautiana katika uwezo wa kuelewa mambo, kujifunza kutokana na uzoefu.
Kikaeleza kuwa hali hiyo huenda sawia na mazingira, kufikiri na kukabili vikwazo vya mawazo. Ripoti hiyo iliongeza kusema kuwa uwezo wa mtu wa kiakili unaweza kutofautiana na mwingine kutokana na matukio pamoja na vigezo mbalimbali.
Katika utafiti mmoja uliofanywa na Lewis Terman mwaka 1921 nchini Marekani kwa ajili ya kubaini watoto wenye akili nyingi, wanafunzi wawili, Wiliam Shockly (mgunduzi wa transistor) na Luis Walter Alvarez walionekana kuwa hawakuwa na uwezo mkubwa kiakili lakini katika utu uzima wao walifanya vizuri sana katika somo la fizikia kiasi cha kutunukiwa tuzo ya Nobel.
Kati ya wanafunzi waliofanya vizuri sana katika utafiti huo, asilimia 30 ya wavulana na asilimia 33 ya wasichana walipokuwa watu wazima hawakuonyesha ubunifu wala uwezo mkubwa wa kiakili na wengine hawakumaliza masomo yao.
Katika kitabu chake kiitwacho ‘Frames of Mind’, mwanasaikolojia Howard Gardner anasema kuwa kuna aina tisa za akili.
Anasema kwamba aina hizi zinaweza kujitokeza wakati wa utoto au ukubwani. Baadhi ya aina za akili ni pamoja na akili ya kujua hesabu, akili ya muziki, akili ya ujuzi wa lugha, akili ya michezo, ujuzi wa uandishi na akili za uvumbuzi wa kisayansi.
Akili nyingine ni za maadili na akili za kujua jinsi ya kuhusiana na watu vizuri.
Zacc Dukowitz katika makala yake inayoelezea jinsi ya kumsaidia kila mwanafunzi kufungulia uwezo wake wa kiakili anasema “Watoto wenye uwezo mdogo kiakili wanaweza kukuza uwezo wao kama watawezeshwa kubadili mtazamo unaowafanya wafikiri kuwa hawana akili.
“Wakisaidiwa kujiona kuwa wana akili, uwezo wao utapanuka na ubongo wao utafanya kazi taratibu lakini kwa hakika kuelekea ufanisi ” anasema Zacc.
Anaongeza kusema kuwa ili mtu amsaidie mtoto awe na akili ni lazima mwenyewe akubali kubadili fikra na mtazamo wake dhidi ya mwanawe kwanza.
Unatakiwa kuacha kusisitiza mtoto kukupatia majibu sahihi bali akupatie mchakato sahihi wa kupata majibu yake.
“Ni vyema kuthamini makosa kama sehemu ya mchakato wa kujifunza na hatimaye kuweza,” naongeza Zacc Dukowitz.
Mmoja wa watu wenye uzoefu katika elimu nchini, Mtemi Zombwe anasema: “Wanaofanikiwa zaidi ni wale wanaoshindwa mara nyingi.”
Katika makala yake iliyochapwa kwenye gazeti hili Agosti 12, mwaka huu kuhusu ‘Shahada bila kujituma ni sawa na umaskini’ anahoji: “Utashindwaje kama hujajaribu mara nyingi?”
Anasema lengo la akili katika maisha siyo kuwakoga au kuwafurahisha wengine kwa kujibu vizuri mitihani bali ni kutuwezesha kukabiliana na changamoto za maisha na kutatua matatizo.
Shule ni sehemu ya maandalizi katika kukuza uwezo wa akili na kumuandaa mtu kujiamini katika fani yake ambayo ataona inamfaa katika maisha yake na kwa jamii nzima.
No comments:
Post a Comment