WANASEMA kama hujui uendako basi walau ujue unakotoka. Naam, naamini hata mkuu wa nchi hajui tuendako kwenye hili la majaribio ya kuandika katiba mpya.
Nina amini kabisa hata mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba naye hajui tuendako katika safari hii ya kupata katiba mpya. Nina sababu za msingi kabisa za kuamini hata wabunge wa Bunge maalum la katiba nao mbele kuna giza kuhusu hatima ya katiba mpya.
Sisi akina yakhe sio tu hatujui tunakoelekea bali tumejawa hofu. Pamoja na kutofautiana na Mwigulu Nchemba katika mambo mengi kimtazamo kwenye siasa za nchi hii, walau sasa nasema kwenye hili la kuona mbali na kiutaka tuangalie ramani kabla ya kwenda tukipapasa ili tujue kama tunafahamu tuendako au la, naungana naye mkono kwa hali zote.
Alichokisema Mwigulu Nchemba kinaweza kuwa hesabu za darasa la tatu au hata la pili. Ni hesabu za kujumlisha, kutoa, kudawanya na kuzidisha.
Anachokisema ni kitu rahisi tu, kama hujui unakokwenda ni afadhali usiende. Na kama unajua unakokwenda na unajua utakwama afadhali ubadili njia urudi ulikotoka.
Ni mtu mpumbavu tu atakayekuwa anasafiri na kuambiwa kilomita kumi mbele barabara haipitiki hivyo vunja safari yako ili usipoteze muda na gharama kusudi ukwame mbele ya safari. Ni mantiki isiyohitaji usomi zaidi ya kufahamu hisabati nyepesi.
Kitendo cha watu kadhaa kutaka wabunge wasitishe bunge hili maalum la katiba vimebeba mantiki kubwa. Naweza kusema baadhi ya sababu huenda haziingii vichwani mwa wale wanaong’ang’ania kuendelea na mchakato kwa sababu Mungu hakuwapa watu wote hekima na uelewa sawa.
Naweza nikawaelewa wale wasioelewa jambo muhimu kama vile katiba ni swala zima la maridhiano. Hivyo wakati wenye hekima wakitaka watu wakae kitako na kutafakari, wapo wanaokimbia ndani ya jengo na kutarajia wingi wao ili kufikia wayatakayo.
Hawa wakati mwingine nawasamehe maana hekima sio kama pumzi ambayo kila mwenye uhai anayo. Lakini hili la kuangalia kwanza idadi ya wanaohitajika kupitisha katiba ili tujue kama akidi itatosha sielewi nini kinawashinda kuelewa hapo.
CRD:TZ DAIMA
No comments:
Post a Comment