Friday, 15 August 2014

MAMA AMUUA MTOTO WAKE KWA MPINI



MKAZI wa Tagamenda nje kidogo ya Manispaa ya Iringa, Habiba Swedi (31), amewafanyia wanawe wawili ukatili wa kutisha kwa kumponda mmoja wa miezi mitatu hadi kumsababishia kifo, huku mwingine wa miaka saba akijeruhiwa vibaya.


Akizungumzia tukio hilo jana, baba yao mzazi wa watoto hao, Bosco Kalolo alisema mwanawe aliyejeruhiwa, amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa akiendelea na matibabu.
“Mimi ni mume wa Habiba, asubuhi ya siku ya tukio tuliamka salama, lakini ghafla mke wangu alipandwa na wazimu na kuchukua mpini wa jembe na kutaka kunipiga nao,” alisema.
Alisema katika purukushani hizo, alifanikiwa kukimbilia nje na ndipo mkewe aliporudi ndani na kuanza kuponda watoto waliokuwa wamelala kitandani kwao kwa huo mpini. Kalolo alisema alilazimika kukimbia kwa sababu alishindwa kukabiliana na mkewe huyo aliyekuwa na nguvu za ajabu.
“Nikiwa nje, nilisikia kitu kikigongwa kwa nguvu na baada ya muda nikasikia sauti ya vilio vikali kutoka kwa watoto na Nilipochungulia, nilimuona mke wangu akiwatwanga watoto hao kwa mpini na ndipo nilipochukua uamuzi wa kuita majirani ili wanisaidie,” alisema.
Alisema kwa msaada wa majirani, walimdhibiti asiendelee kufanya kitendo ambapo walimkamata na kumpeleka Polisi, kabla ya kupelekwa hospitalini anakoendelea kuangaliwa chini ya ulinzi.
Kalolo alisema yeye na mke huyo wamedumu katika maisha yao ya mume na mke kwa miaka 10 na kufanikiwa kupata watoto wanne.
Mratibu wa Afya na Akili wa Hospitali hiyo, Dk Alli Ngalla alisema mama huyo anayeonekana kuwa na tatizo la ugonjwa wa akili wa mara kwa mara (kichaa), amelazwa katika wodi ya vichaa hospitalini hapo akiwa hajui kinachoendelea.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema limetokea Agosti 14 saa 12 asubuhi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.
Akizungumzia sakata hilo, Dk Ngalla alisema uchunguzi wa awali unaonesha kwamba mwanamke huyo ana matatizo ya akili kwa muda mrefu lakini hajawahi kutibiwa katika kituo chochote cha afya.
“Alikuwa akitibiwa kwa tiba asilia na kupitia maombi ya kanisani jambo lililosababisha tatizo kuendelea kukua siku hadi siku,” alisema.
Ngalla alisema laiti kama ndugu wangemwahisha mapema katika vituo vya kutolea huduma za matatizo ya akili huenda yaliyotokea yasingetokea.
“Mwito wangu kwa watu wanaoishi na ndugu au jamaa zao wenye matatizo ya akili wawawahishe hospitalini, ili wachunguzwe na kuanza kupewa huduma,” alisema. Alisema baadhi ya watu wameingia kwenye magonjwa ya akili kwa sababu ya kukabiliwa na msongo wa mawazo.

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!