BAADA ya kuwaona magwiji wa Real Madrid wakiongozwa na Luis Figo, sasa mashabiki wa soka wa Tanzania watakishuhudia kikosi cha sasa cha timu hiyo bingwa wa bara la Ulaya.
Juzi Jumamosi, Figo akiwa na mwanasoka mwingine mahiri wa zamani duniani, Fabio Cannavaro, walicheza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mbele ya maelfu ya mashabiki. Katika pambano hilo la kimataifa la kirafiki dhidi ya kikosi cha wakongwe nchini, Tanzania XI, Real Madrid walishinda mabao 3-1.
Baada ya kuvutiwa na mchezo huo uliowagusa maelfu ya Watanzania ambao uliratibiwa na Kampuni ya TSN Supermarkets, Real Madrid ya sasa inaletwa nchini kama magwiji hao.
Rais Jakaya Kikwete aliyeshuhudia pambano hilo akitokea safarini kikazi mikoa ya Morogoro na Arusha, ameweka wazi kuwa mipango ya kuwaleta kina Cristiano Ronaldo, Gareth Bale, James Rodriguez na wengine imeanza.
“Watanzania wamefurahishwa sana na kuja kwenu pamoja na pambano safi walililoona jioni ya leo (juzi) pale uwanjani.
“Sasa tunataka ije timu ya sasa ya Real Madrid. Nimezungumza na Balozi (wa Hispania nchini), atasimamia jukumu hilo,” alisema Rais Kikwete, juzi usiku Ikulu katika chakula cha usiku alichokiandaa kwa timu hizo mbili.
Balozi wa Hispania nchini, Luis Manuel Civis, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo.
Rais Kikwete ambaye chini ya utawala wake, amekuwa mstari wa mbele kusaidia sekta ya michezo, alisema mashabiki wa soka na Watanzania kwa ujumla waliojitokeza Taifa, wamefurahishwa sana na pambano hilo la juzi.
Aidha, Rais Kikwete alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Real Madrid utaendelezwa zaidi kwa kuhakikisha miamba hiyo inajenga kituo chake cha mafunzo ya soka kwa vijana.
Magwiji hao wa zamani mbali ya kupata fursa ya kula chakula na Rais Kikwete na viongozi wengine wa Serikali, pia Rais aliwapa kila mmoja zawadi ya kinyago cha Kimakonde.
Awali, Figo na wenzake akiwamo nahodha wa Italia aliyetwaa Kombe la Dunia 2006, Fabio Cannavaro walimkabidhi Rais jezi iliyosainiwa na wachezaji wa timu hiyo bingwa wa Ulaya.
Aidha, wachezaji hao walimpatia pia jezi kama hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TSN Supermarkets, Farough Baghozah, ambaye amefanikisha ziara hiyo ya kwanza ya aina yake kwa miamba hiyo Tanzania na barani Afrika.
Magwiji hao wa Real Madrid jana walitarajiwa kutembelea mlima Kilimanjaro mjini Moshi na leo watakuwa Arusha kutembelea kreta ya Ngorongoro kabla ya kurejea makwao kesho
HABARI LEO.
No comments:
Post a Comment