RAIS Jakaya Kikwete anatarajia kufungua kikao cha tatu cha Bunge la Tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), litakaloanza kesho kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam. Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Spika wa EALA, Margaret Nantongo Zziwa alipozungumza na waandishi wa habari.
Zziwa alisema katika kipindi cha wiki mbili, Bunge hilo litapitia hoja, maazimio na maswali mbalimbali ambayo yatakuwa yameletwa kwenye mkutano na kupokea na kujadili ripoti kutoka Kamati mbalimbali za Bunge.
Alizitaja ripoti hizo kuwa ni ya Kamati ya Masuala ya Jumuiya na Upatanishi wa Migogoro na Kituo cha Uongozi cha Afrika cha Taasisi za Afrika Mashariki na Usalama wa Jumuiya.
Alisema Bunge pia litapokea ripoti ya Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili kuhusu semina ya Wabunge wa Jumuiya juu ya Misitu na Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Ripoti ya Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji kuhusu Sekta ya Urafiri wa Anga ya EAC.
Akizungumzia miswada mbalimbali, Zziwa alisema Bunge litapokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu Muswada wa Elimu kutoka Kamati ya Masuala ya Jumuiya na Upatanishi wa Migogoro.
Alisema kuhusu Muswada wa Masuala ya Ushirika, Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili inayoshughulikia muswada huo inatarajia kuanza vikao vya wazi wakati muswada wa Masuala ya Biashara uko mbele ya Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji.
Aidha, Zziwa alisema pamoja na vikao Wabunge wa EALA watapata fursa ya kutembelea Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) ili kuongeza ushirikiano na wadau na kuboresha kazi ya utungaji wa sheria.
Kwa sasa Jumuiya imeshapita mchakato wa utengamano kwa kutekeleza Itifaki mbalimbali, ikiwamo ni Umoja wa Forodha, Himaya Moja ya Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Forodha, ambao Tanzania imekuwa nchi pekee iliyoridhia itifaki hiyo.
Zziwa alisema kuwa utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha unatarajia kuanza mara baada ya nchi zote wanachama kuidhinisha itifaki hiyo ambayo mpaka mwishoni mwa mwaka huu nchi wanachama wanatakiwa kuwa wameridhia.
“Hii ni hatua muhimu sana ambayo itasimika mchakato huu wa utengamano, utekelezaji wake utahitaji kuwepo kwa sheria mbalimbali, EALA tumejizatiti kuhakikisha kuwa tunatunga sheria.
“Natoa mwito kwa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki kuleta hii miswada kwenye Bunge haraka iwezekanavyo.”
Aidha, Zziwa alisema pamoja na hatua iliyopigwa katika mtengamano, lakini kumekuwa na changamoto kadhaa na kutaka vikwazo vya kibiasha visivyo vya kiforodha (vinashughulikiwa kikamilifu.
Alisema changamoto nyingine ni pamoja na kusuasua kwenye utekelezaji wa ajenda ya EAC kwenye sera za taifa za nchi wanachama wa Jumuiya.
Zziwa alitoa shukrani kwa Rais Kikwete, na Serikali kwa kukubali kuwa mwenyeji na kutokana na uongozi wake mahiri na mchango wake kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hii ni mara ya kwanza kwa Bunge la Tatu kufanya mkutano wake Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kufanya vikao kwa zamu kwenye nchi zote wanachama ili kuliweka Bunge kuwa karibu zaidi na wananchi na wapate fursa kufahamu kuhusu shughuli za EALA.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment