RAIS Jakaya Kikwete, ameagiza mamlaka zote za uhakiki wa mipaka na uwekaji mawe katika Mpaka wa Kimataifa wa Tanzania na Burundi na mipaka na nchi nyingine, kukamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo.
Aidha, amesema kuwa Tanzania inapima mpaka wake na Burundi na mipaka yake na nchi nyingine jirani, si kwa sababu ya kuwepo kwa migogoro na nchi jirani, bali kwa sababu ya kuwahakikishia wananchi wa nchi zote kufahamu ni sehemu gani na mazingira yapi wanafanyia shughuli zao za maendeleo.
Rais Kikwete ameungana na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza juzi kuzindua kazi ya upimaji na uwekaji mawe ya mpaka kati ya Tanzania na Burundi, katika sherehe kubwa na ya kusisimua iliyofanyika upande wa Tanzania wa kijiji cha mpakani cha Mugikomero.
Aliwasili Mugikomero saa 8:15 mchana, akitokea Uwanja wa Ndege wa Mchauru, mjini Geita, ambako ndege yake ilitua saa nne kamili asubuhi, ikitokea mjini Dodoma na kujiunga na Rais Nkurunzinza ambaye alitangulia kuwasili kwenye kijiji hicho.
Rais Kikwete ameelezea uzinduzi huo kuwa kielelezo tosha cha uhusiano mwema, udugu na urafiki uliopo kati ya Tanzania na Burundi; nchi mbili ambazo pamoja na Rwanda zilikuwa nchi moja chini ya utawala wa Wajerumani ulioitwa German East Africa.
Nchi hizo zilitengana baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambapo Tanganyika iliwekwa chini ya utawala wa Waingereza wakati Burundi na Rwanda ziliwekwa chini ya himaya ya Ubelgiji.
Akizungumzia umuhimu wa kuhakiki mpaka, Rais Kikwete alisema mara ya mwisho kwa mpaka wa Kimataifa wa Tanzania na Burundi kuhakikiwa na mkataba kusainiwa kati ya nchi hizo, ilikuwa Agosti 5, 1924; miaka 90 iliyopita.
“Kama zilivyo nchi nyingine za Afrika, Tanzania na Burundi zilirithi mpaka uliopo kutoka kwa waliokuwa watawala wetu enzi za ukoloni. Mpaka huu haujafanyiwa marekebisho wala kuimarishwa tangu nchi zetu zipate uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita.
“Katika kipindi hicho, yamekuwepo mabadiliko mengi ikiwemo ongezeko la watu, shughuli za maendeleo katika maeneo ya mpakani na hata alama za mipaka zimekuwa vigumu kutambulika, ama kwa sababu ya kuchakaa au mawe yameng’olewa,” amesema Rais Kikwete.
Aliongeza pia kuwa baada ya kutambua vyanzo vya migogoro na utata miongoni mwa baadhi ya nchi za Afrika, Umoja wa Afrika (AU) katika Kikao cha Wakuu wa Nchi za Serikali kilichofanyika Accra, Ghana Juni 2007, iliamuliwa kuwa nchi zote zishirikiane kuimarisha mipaka yao ifikapo 2012. Muda huo uliongezwa hadi 2017.
Rais Kikwete alisema kuwa zoezi hilo ambako katika awamu ya kwanza kilometa 120 za mpaka zimepimwa na kuwekewa mawe ya utambuzi wa mpaka, halikuwa rahisi kwa sababu mpaka wa Tanzania na Burundi ni mrefu, kiasi cha kilometa 450, sawa na urefu kati ya Dar es Salaam na Lindi.
“Isitoshe mpaka hauko mijini, maeneo mengi yako misituni kwenye mabonde na milima. Ni vigumu kuyafikia. Kwa upande wetu, mpaka uko katika mikoa miwili ya Kagera na Kigoma na katika wilaya tano, nne zikiwa katika Mkoa wa Kigoma na moja ikiwa Ngara, Mkoa wa Kagera. Isitoshe, hatuna mfadhili na zoezi hili tumeligharimia sisi wenyewe,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema kuwa mbali na Burundi, Tanzania inaendelea na upimaji kwa nchi nyingine jirani na kuongeza kuwa mpaka wa Tanzania na Kenya, Msumbiji na Comoro na Shelisheli katika Bahari ya Hindi imekamilika na mikataba imesainiwa.
No comments:
Post a Comment