Wakati wanaharakati duniani wakitaka hukumu ya kifo ifutwe, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amir Manento amesema muda wa Tanzania kufuta hukumu hiyo haujafika na kwamba endapo uamuzi huo utatekelezwa mauaji yataongezeka.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Manento alisema kuwa kinachotakiwa kufanyika ni kubadilishwa kwa sheria ya hukumu ya kifo, ili itoe nafuu kidogo kwa watuhumiwa kuliko ilivyo hivi sasa. “Yaani adhabu ibaki pale pale, watu watakuwa wanaogopa ogopa ‘bwana utanyongwa’. Sheria itamke kama rais hatasaini hukumu kwa miaka 30, mtuhumiwa awe na matumaini ya kuachiwa huru,” alieleza.
Wakati Manento akizungumza hayo, zaidi ya wafungwa 300 wapo katika magereza mbalimbali nchini wakisubiri kuvalishwakitanzi cha kunyongwa wakati wowote rais atakaposaini hukumu zao. Manento alisema kwamba baadhi ya watu waliohukumiwa kunyongwa, wanaweza kuua watu wengi zaidi iwapo wataachiwa huru, pia watakuwa katika hatari ya kupigwa na wananchi.
Akitoa mfano alisema kuwa mwanamke mmoja aliyefikishwa mahakamani hivi karibuni kwa kosa la kumchoma moto msichana wake wa kazi za ndani, wanawake waliokuwa nje ya mahakama hiyo walitamani waruhusiwe kumwadhibu kutokana na hasira walizokuwa nazo.
Hata hivyo, alisema kuwa baadhi ya wananchi wameacha kuwaonea huruma watoto na ndugu, ambao wameachwa pekee yao baada ya wazazi wao kuuawa kwa makusudi, badala yake wanawaonea huruma waliofanya makosa.
“Mimi nafikiria wakati bado (wa kufuta hukumu ya kifo), kati ya nchi 52 za Marekani ni sita tu ambazo zimeondoa adhabu ya kifo. Afrika Kusini kuna jaji alilalamika sana alisema anatamani ile hukumu ingekuwa haijafutwa, kutokana na ukatili alioufanya muuaji,” alisema Jaji Manento.
Alisema ingawa kuna taasisi na mashirika yanayosema kutokutekelezwa kwa hukumu ya kifo kunawapa matatizo ya kisaikolijia waliohukumiwa kunyongwa, lakini idadi kubwa ya ndugu wa watu waliouawa wanataka adhabu hiyo.
No comments:
Post a Comment