PAMOJA na kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa mwenye virusi vya homa hatari ya ebola, wala anayehisiwa kuwa na ugonjwa huo nchini, Serikali imeshajiandaa kukabiliana na ugonjwa huo, ambao umeshaua zaidi ya watu 1,000 katika nchi za Afrika Magharibi.
Katika maandalizi hayo, Serikali imeagiza vituo kadhaa katika mikoa yote, kuwa tayari kutoa huduma endapo atatokea mgonjwa aliyepata maambukizi ya ugonjwa huo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu hatua hizo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema katika vituo hivyo vifaa kinga pamoja na dawa vimeshaandaliwa.
“Katika Mkoa wa Dar es Salaam, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Temeke Isolation Unit, yametengwa maeneo ya kuhudumia wagonjwa wa ebola endapo watatambuliwa. Eneo la Temeke bado linaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia vigezo maalumu ili likidhi mahitaji ya matibabu ya ugonjwa huu,” alisema Dk Rashid.
Alisema wizara hiyo, pia imetoa mwongozo kwa maeneo yaliyoainishwa katika mikoa yote Tanzania Bara, kuandaa sehemu ya kutenga wagonjwa wakati wa matibabu na itahakikisha kuwa maeneo hayo yanakuwa na vigezo vinavyohitajika.
Ingawa hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya ebola hapa nchini, lakini hatua hizo zimechukuliwa kwa tahadhari, kwa sababu kwa mujibu wa Dk Rashid, magonjwa hayatambui mipaka ya nchi.
Akizungumzia tahadhari hizo, Dk Seif alisema pamoja na kutenga maeneo hayo, pia Serikali imeunda kikosi kazi kinachohusisha wajumbe mbalimbali wakiwemo wadau wa maendeleo na watendaji wengine, kwa ajili ya kuandaa kwa kina hatua za dharura zinazotakiwa kudhibiti ugonjwa huo.
Wadau hao waliomo katika kikosi kazi hicho ni Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Msaada la Marekani (USAID), Shirika la Maendeleo la Kikoloni (CDC) na watendaji wengine kutoka taasisi za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
“Kikosi hiki kimeshakutana mara nne kwa ajili ya kuandaa kwa kina hatua za dharura zinazotakiwa kuchukuliwa, ili kudhibiti ugonjwa huu usiingie hapa nchini. Tayari kikosi hiki kimeandaa Mpango wa Dharura wa kukabiliana na ugonjwa wa ebola kuanzia ngazi ya Taifa hadi wilaya,” alisisitiza.
Alisema mpango huo unaainisha maeneo mbalimbali, ikiwemo ufuatiliaji wa ugonjwa huo, namna ya kutambua na kuchukua sampuli, matibabu ya wagonjwa, mwongozo wa namna ya kutenga sehemu maalumu, uelimishaji wa umma na ushirikishwaji wa wadau wengine mbalimbali katika kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa ebola.
Dk Seif pia alisema kikosi kazi hicho kitatumika kutoa tahadhari kwa umma, kuhusu tishio la ugonjwa huo ambapo tayari tahadhari hiyo ilitolewa Agosti 2, mwaka huu kupitia vyombo vya habari.
Tahadhari hiyo ilitolewa Agosti 2, 2014 kupitia vyombo vya habari, ambapo iliainisha namna ya kutambua ugonjwa huo, umuhimu wa kuwahi matibabu, jinsi ya kujikinga na pia hatua gani zinatakiwa kutekelezwa na jamii ili kudhibiti ugonjwa hio.
*Mipakani Pamoja na hayo, alisema Serikali katika kuendelea kuchukua tahadhari, pia imeboresha ufuatiliaji na utambuzi wa ugonjwa huo katika maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani ili kubaini wasafiri watakaoonesha dalili za ugonjwa au wenye viashiria hatari.
Alisema fomu maalumu za kuhoji wasafiri, zimeanza kutumika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na wa Kilimanjaro (KIA) kuanzia Agosti 5, mwaka huu ambazo pia zitatumika katika maeneo yote ya mipakani.
“Orodha ya abiria kwenye ndege pia imeanza kutumika, ili kutambua abiria wanaoingia nchini na kuainisha nchi walizotoka kabla ya ndege kutua nchini,” alisema.
Alisema Wizara pia imeagiza mashine aina ya “Thermoscanners” zitakazowekwa katika viwanja vyote vya ndege, kwa ajili ya kurahisisha utambuzi wa wasafiri watakaokuwa wanaingia nchini na kuwa na dalili za mwanzo ambayo ni homa.
“Wasafiri wanaoondoka watapewa vipeperushi vya kuelimisha. Katika viwanja hivi, vifaa kinga vimesambazwa kwa ajili ya watumishi wa afya,” alisisitiza.
Aliwatoa hofu wananchi kuhusu ugonjwa huo na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari, huku akisisitiza kuwa ebola inazuilika endapo watu wataepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini kwa mtu mwenye dalili za ugonjwa huo kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.
Aidha aliwataka kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa huo, na badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha huduma za afya kwa ushauri, ili kuruhusu wataalamu kusimamia maziko ikiwa itatokea.
Dalili za awali za ugonjwa huo ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni.
Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, kutokwa na vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa, hutokwa damu ndani na nje ya mwili.
Ugonjwa wa ebola hauna tiba maalumu wala chanjo. Hata hivyo mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili atakazokuwa nazo.
Katika hatua nyingine, vipimo vya watu wawili waliohisiwa kuwa na ugonjwa huo Uganda na Rwanda, vimebaini kwamba hakuna hata mmoja wao aliyeambukizwa ugonjwa huo.
Waziri wa Afya wa Rwanda, Agnes Binagwaho alisema jana kuwa mwanafunzi mmoja wa Ujerumani, aliyefika nchini humo akitokea Liberia, ambayo ni miongoni mwa nchi nne za Afrika Magharibi ambazo virusi vya ebola vimeenea, alihisiwa kuwa na ugonjwa huo, lakini baada ya sampuli ya damu yake kupimwa katika maabara za kimataifa, hakukutwa na ugonjwa huo.
Msemaji wa Wizara ya Afya wa Uganda, Rukia Nakamatte, naye mwishoni mwa wiki alitoa taarifa kwamba mtu mmoja nchini humo aliyekuwa amewekwa katika chumba cha pekee baada ya kuwa na homa, baada ya kupimwa hakukutwa na virusi vya ebola.
VIA-HABARI LEO
No comments:
Post a Comment