HOFU ya kuenea kwa kasi ugonjwa hatari wa ebola imeendelea hasa mkoani Kigoma ambao uko mpakani baada ya taarifa kuwa umeishaingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo inapakana.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya, alisema kwa sasa walishaanza kuchukua tahadhari katika mipaka yote, pia wataalamu wameishatawanywa wilaya zote sanjari na vifaa vya uchunguzi kabla ya watu hawajaingia nchini.
Alisema walishapata maelekezo kutoka Wizara ya Afya, ambako walishaanza kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuchukua tahadhari kuhusu ugonjwa huo sambamba na kutoa taarifa endapo atatokea mtu atakayeonyesha kuwa na dalili za ugonjwa huo.
“Tuko makini sana katika kupambana na ugonjwa huu, kwani tutaanza kampeni leo hii ya kuwatangazia wananchi kwa kutumia vipeperushi na magari ya vipaza sauti, ambayo yatapita kila mtaa usiku na mchana,” alisema Machibya.
Aidha, Katibu Tawala wa Mkoa, John Ndunguru, alisema kwa sasa njia zote kuanzia uwanja wa ndege, bandarini na barabara ambazo ziko mpakani, kuna maofisa wa afya ambao hufanya kazi ya kutoa elimu na kuchunguza kila anayeingia kama ana dalili za ugonjwa huo.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa, Leonard Subi, alipoulizwa kama alipokea vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo, alikiri kupokea na kuongeza kuwa bado wanasubiri vingine ili kuongeza ufanisi katika harakati za kudhibiti ugonjwa huo.
“Kwa sasa ukienda ‘airport’ hata bandarini, utakuta vifaa vya kujilinda sambamba na maofisa wa afya ambao huwachunguza watu wote wanaoingia,” aliongeza Subi
No comments:
Post a Comment