Siku chache baada ya kusambaa kwa taarifa juu ya uwepo wa majambazi wanaotumia pikipiki katika maeneo ya Mlimani City na Millennium Tower, mfanyabiashara mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi siku ya Ijumaa katika eneo la Mlimani City.
Edson Cheyo, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Sowers African iliyopo jirani na Mlimani City, alifikwa na umauti baada ya kuchukua fedha benki. Inadaiwa baada ya kutoka benki watu waliokuwa katika pikipiki walimpiga risasi na kuondoka na fedha zote alizokuwanazo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema Cheyo alipigwa risasi mbili kifuani na begani, lakini alifariki dunia njiani alipokuwa akipelekwa Hospitali ya Mwananyamala.
Wambura alisema watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, waliondoka na fedha alizokuwa nazo marehemu, kiasi kinachodaiwa kuwa ni Sh.18 milioni. Hata hivyo, alisema Polisi hawakuweza kuwakamata, bado wanaendelea kuwasaka.
“Kila siku tunawaambia wananchi wawe wanaomba ulinzi wa Polisi wanapobeba kiasi kikubwa cha fedha, matukio kama haya hayawezi kutokea. Jeshi la Polisi lipo kwa ajili yao, ni vyema wakalitumia kwa ulinzi wao na mali zao,” alisisitiza Wambura.
Awali, taarifa zilienea katika mitandao ya kijamii kuwa majambazi wanaotumia pikipiki wameweka kambi katika maeneo ya kibiashara yenye mikusanyiko ya watu ambapo hupora fedha na kuwadhuru watu.
Taarifa hiyo ilitaja maskani ya majambazi hayo kuwa ni nje ya jengo la Millennium Tower, eneo la Mlimani City na sasa wameweka kambi katika jengo la Kibo Complex.
“Muwe na tahadhari mnapoenda Millennium Tower hasa kufanya shughuli za kifedha. Kuna majambazi wa pikipiki wana kijiwe hapo na polisi wanajua. Pia, Mlimani City nayo ni kambi yao na sasa wameanzisha nyingine Kibo Complex,” ilisomeka taarifa hiyo katika mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, Mwananchi lilipofanya uchunguzi wa awali juu ya uwepo wa vijana hao katika maeneo tajwa, hapakuwa na dalili na wala haikujulikana wanafanya shughuli zao za kihalifu wakati gani.
Kamanda Wambura alikanusha habari hizo na kudai kuwa hakuna majambazi walioweka kambi katika maeneo yanayoelezwa kwani walishafanya uchunguzi na bado wanaendelea na doria ya mara kwa mara katika maeneo hayo na mengine.
No comments:
Post a Comment