Monday, 25 August 2014

DALADALA 1800 ZAJIOKOA KWA KUUNGANA NA UDA


UWEZEKANO wa kufa kwa sehemu kubwa ya biashara ya daladala jijini Dar es Salaam umepungua, baada ya wamiliki wa biashara hiyo kuingia mkataba na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), ili kuendesha Mradi wa Mabasi ya Kasi Dar es Salaam (DART).



Kabla ya mkataba huo wa juzi Jumamosi, mradi wa Dart ulipanga kuondoa mabasi zaidi ya 1,800 katika barabara zenye abiria wengi na kupelekwa katika barabara za pembezoni.
Utiaji saini wa mkataba huo ulifanyika Dar es Salaam juzi na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
Hivi karibuni kabla ya kuibuka kwa mpango wa kuunganisha nguvu ya wazawa na kusainiana mkataba huo, Meneja Uendeshaji wa Dart, Peter Munuo alisema daladala hizo zinazofanya safari zake kati ya Kimara na Kivukoni, zinatarajiwa kuondolewa katika barabara hiyo yenye wateja wengi, baada ya kuanza kwa awamu ya kwanza ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (Dart).
Daladala hizo kwa mujibu wa Munuo, zilitarajiwa kupangiwa njia nyingine za pembezoni, ambako hakuna wateja, kama barabara za awali, huku madereva wake watakaojitokeza kuomba ajira, wakipewa kipaumbele katika mabasi ya kasi yatakayorithi barabara hizo.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, alinukuliwa akisema, daladala za sasa zitaondolewa katika zaidi ya njia 43, ambazo ziko kwenye barabara ya Morogoro na barabara ya Kawawa na katika ruti nyingine.
Alisema daladala hizo zitaendelea kuondolewa hadi hapo ujenzi wa barabara zote za Dart utakapokamilika.
Kwa mujibu wa Meneja Msimamizi wa Matumizi ya Barabara wa Dart, Mohamed Kuganda, mradi huo wa mabasi ya kasi, unatarajiwa kukamilika mwaka kesho chini ya mkandarasi aliyepewa zabuni hiyo, Kampuni ya Strabag.
Baada ya utiaji saini wa mkataba huo kati ya wamiliki wa daladala na Uda, Waziri Ghasia alisema uamuzi huo ni mfano wa kuigwa nchini. Alisema kuungana kwao pamoja kutawajengea mazingira bora ya kuaminika zaidi, ambayo yatatoa ushindani madhubuti dhidi ya kampuni za nje zitakazojitokeza kuomba kuendesha mradi huo wa Dart.
Pia alimpongeza Mwenyekiti wa Saimon Group, Robert Kisena na viongozi wa vyama vya wamiliki wa daladala Mkoa wa Dar es Salaam, kwa uamuzi huo wenye tija kwa Taifa kwani utaongeza ajira zaidi na kupunguza umasikini.
Uamuzi huo ulifikiwa baada ya mkutano uliofanyika Ijumaa iliyopita jijini Dar es Salaam, ulioandaliwa na Kamati Teule ya Wamiliki wa Daladala na kuwakutanisha wamiliki wote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki alisema kuunganisha nguvu kwa wadau hao, kutatoa fursa kwa Serikali kuwaunga mkono katika jitihada zake za kuboresha hali ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
“Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na wazawa, kwani haiwezi kutumia mabilioni kujenga barabara hizo halafu kweli eti mtu wa kuziendesha atoke nje... hii itakuwa aibu na dharau.
“Haiwezekani... kuungana kwenu kutaishawishi Serikali zabuni zitakapotangazwa, ili mfikiriwe kupewa kipaumbele kwani najua kuungana kwenu ni ishara kwamba mmedhamiria kupambana katika zabuni hizo,” alisema Sadiki.
Naye Kisena alisema watafungua milango kwa wamiliki hao kununua hisa zitakazowezesha mtu yeyote kuwa Mkurugenzi.
“Pia tunatoa mwito kwa wananchi mbalimbali kujitokeza kununua hisa kwa wingi zaidi, ili kuhakikisha tunaboresha huduma ya usafiri katika jiji hili,” alisema Kisena.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk alisema kutokana na Uda kuwa kampuni yenye uwezo, kuna haja ya kuunganisha nguvu kwa pamoja ili kuhakikisha zabuni itakapotangazwa, hakuna kampuni kutoka nje itakayoshinda.
“Hakuna sababu yoyote ya kumwachia mtu kutoka nje kuja kuendesha mradi huu, tukikusanya mitaji na kuungana na Uda, tuna hakika tutaweza kuendesha mradi huu kwani hauhitaji fedha nyingi sana na sisi tukiamua tunaweza,” alisema Mabrouk.
Tayari taarifa zinaonesha kuwa mradi huo utakapoanza, nauli ya basi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kwenda na kurudi vituo vikubwa vikiwemo vya Kariakoo na Posta, itapanda kutoka nauli ya chini ya Sh 400 ya sasa mpaka kati ya Sh 700 na Sh 800 kwa ruti moja.
Kwa wanafunzi, nauli kwa ruti moja kwenda katika vituo hivyo vikubwa katika mradi huo ambao utaanza kwa majaribio mwishoni mwa mwaka huu, zitapanda kutoka Sh 200 mpaka nusu ya nauli ya mtu mzima kwa ruti husika.
Aidha, mfumo wa uendeshaji wa mradi huo na nauli, umewekwa katika sehemu mbili; sehemu ya kwanza ni usafirishaji wa abiria kutoka maeneo ya ndani ya makazi ya watu mpaka katika vituo vidogo na vikubwa vilivyopo barabara kuu za Dart za Morogoro na Kawawa kwa sasa.
Sehemu ya pili ni usafirishaji wa abiria kutoka katika vituo vilivyopo katika Barabara Kuu za Dart za Morogoro na Kawawa, kwenda vituo vikuu vikiwemo Kariakoo na Posta.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, abiria atakayelazimika kusafiri na mabasi ya Dart kwa safari fupi ndani ya barabara zilizo katika makazi ya watu, kwa mfano wa barabara inayopita Sinza; kutoka Bamaga mpaka Shekilango, atalipa Sh 500, tofauti na sasa ambapo analipa Sh 400.
Kwa atakayetumia mabasi ya Dart kutoka katika barabara ndogo zilizopo katika makazi ya watu, kwenda katika vituo vikubwa vya Dart vilivyopo njia kuu za Morogoro na Kawawa ili kwenda Kariakoo, Posta au Kimara, atalazimika kukata tiketi ya Sh 800, atakayoitumia kupata usafiri kutoka barabara ndogo na katika barabara kubwa.
Mfano wa nauli hiyo, ni abiria anayetoka maeneo hayo ya Sinza kwenda Kimara, Kariakoo au Posta, ambaye atalazimika kukata tiketi ya Sh 800, itakayomwezesha kupakia basi la Dart kutoka maeneo hayo mpaka Shekilango, ambako atabadilisha basi kwa tiketi hiyo hiyo, kwenda Kariakoo, Posta au Kimara.
Aidha, kwa abiria watakaolazimika kutumia mabasi matatu ya Dart, kutoka katika barabara ndogo zilizopo katika makazi ya watu, kupitia barabara kuu za Dart na kwenda katika eneo lililopo katika barabara ndogo za makazi ya watu, watalazimika kulipa Sh 900 kwa mabasi yote matatu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!