Mazishi ya ya aliyekuwa msaidizi wa Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Efatha, Nabii Josephat Mwingira, marehemu Adson Philip Cheyo yakiendelea.
Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Efatha, Nabii Josephat Mwingira, mwishoni mwa wiki alimpoteza mkalimani wake, Adson Philip Cheyo aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, Cheyo alikuwa ametoka katika mojawapo ya matawi ya benki mbalimbali zilizopo eneo hilo lenye shughuli nyingi zilizojaa pilikapilika, akiwa na kiasi cha fedha zinazokadiriwa kuwa shilingi milioni nane.
Mwili wa marehemu Adson Philip Cheyo ukiwa kwenye jeneza.
Baada ya kuchukua fedha hizo, inadaiwa kuwa mkalimani huyo ambaye hutumiwa zaidi na Nabii Mwingira anapokwenda kuhubiri nje ya nchi, alikwenda sehemu aliyoegesha gari lake na kuingia, lakini kabla hajafanya chochote, vijana wawili walitokea na kumtaka awape fedha alizoshika, kitendo ambacho alikitii.
Lakini pamoja na kuwapa fedha hizo, vijana hao walimpiga risasi mbele ya mke wake na kuondoka bila kukamatwa, kitu kinachotia shaka kubwa juu ya usalama wa eneo hilo lenye kutembelewa zaidi na watu wenye fedha jijini Dar es Salaam.
Katika ibada ya kumuombea marehemu wakati akiagwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Mbeya, Nabii Mwingira alisema kifo hicho ni pigo kubwa kwake na waumini wenzake, lakini wanaamini kilichotokea ni mapenzi ya Mungu na wao watamuombea kila mara.
Waumini wengine wa kanisa hilo walionekana kuwa na majonzi, hasa kutokana na kuwa karibu na marehemu huyo, aliyezaliwa Januari 7, 1970.
No comments:
Post a Comment