Friday, 11 July 2014

WATUHUMIWA WA MLIPUKO WAPEWA HATI YA MASHITAKA

Watuhumiwa milipuko wapewa hati ya mashitaka
WASHITAKIWA wanaosadikiwa kujihusisha na makundi ya kigaidi nchini likiwemo la Al-Shabaab, wanaodaiwa kuhusika na mlipuko kwenye baa ya Arusha Night Park wamepatiwa hati ya mashtaka yanayowakabili (charge sheet).

Watuhumiwa hao, walipewa hati hiyo na mwanasheria wa Serikali, Gaudencia Joseph mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Msofe jana.
Hatua hiyo, inatokana na maombi yaliyowasilishwa na washtakiwa hao tisa mahakamani hapo Juni 11 mwaka huu, wakati shauri hilo lilipofika kwa ajili ya kutajwa, wakiomba wapatiwe hati hizo ili wajue wanashtakiwa kwa makosa gani.
Mwanasheria wa Serikali, Joseph, aliieleza mahakama hiyo kuwa, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo kuomba liahirishwe hadi Julai 24 mwaka huu litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa kwenye shauri hilo namba 43 la mwaka 2014 ni pamoja na Abdallah Athumani, Abdalah Maginga, Hassan Zuberi Saidi, Ally Hamisi Jumanne, Yasin Sanga, Shaban Wawa, Abubakar Thabit, Abdalah Yasin na Sudi Nasib.
Awali ilielezwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kutishia kuua, kuwashawishi na kuwasafirisha vijana kwenda nje ya nchi kupata mafunzo ya kigaidi, ambapo ni kinyume na kanuni namba 21 (a), sheria ya kuzuia ugaidi ya mwaka 2002.
TZ-DAIMA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!