Friday, 25 July 2014
WANAOTUMIA SARE NA VIFAA VINGINE VYA JESHI-KUKIONA"
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeonya juu ya matumizi ya sare na vifaa vingine vya majeshi kwa watu wasiohusika. Limetangaza kuwa hatua kali za kisheria, zitachukuliwa dhidi ya watu hao.
Limehadharisha juu ya uvaaji, uingizaji nguo nchini ikiwemo mitumba, kwamba kama itatokea, zinafanana kwa aina yoyote ile na ikadhaniwa ni za jeshi hilo, mtu anayehusika atafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu sare za majeshi zilizopo.
“Msisitizo uliwekwa hapa katika vifungu vya sheria ni kwamba sio lazima ukutwe na sare ambazo zinatumiwa na JWTZ. Hasha!. Hapa sheria inasema hata kama tu nguo hiyo itaelekea kufanana kwa namna yoyote ile na sare za JWTZ, ni kosa la kisheria kuitumia,” ilisema taarifa ya Jeshi kwa vyombo vya habari.
Taarifa hiyo ilitolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano, Makao Makuu ya Jeshi, jijini Dar es Salaam, jana. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtu yeyote yule asiye na ruhusa ya kushona, kuuza au kuingiza nchini sare za jeshi, atakuwa ametenda kosa, hivyo atafikishwa mahakamani.
Tamko hilo la jeshi linasema kwa muda mrefu sasa katika miji mikubwa, hasa Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma na mikoa mingine, kumekuwa na ongezeko la matukio ya wizi na uhalifu wa kutumia silaha.
“Imeonekana kuwa wanaohusika na vitendo hivyo, baadhi yao huonekana wamevaa sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na zimekuwa zikitumika katika matukio yenye sura ile ile,” ilisema.
Taarifa hiyo ilisema, “Hivi karibuni vichwa vya habari vimetawala sana kwenye vyombo mbalimbali vya habari sehemu mbalimbali hapa nchini, mara utasikia ‘Mwanajeshi feki mbaroni Tanga’ au Aliyejifanya Ofisa wa JWTZ akamatwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na mengine mengi.”
Ilisema pia kumejitokeza mtindo wa baadhi ya wasanii hasa wanamuziki wa kufokafoka maarufu bongo fleva, kurekodi video zao wakiwa wamevaa sare za jeshi, kama vile suruali, viatu, fulana, kaptula, mabegi au kofia.
Kulingana na taarifa hiyo, mitaani nako kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi, hasa vijana, wanaovaa sare za jeshi, ambao wakiulizwa wanakozitoa, hudai wamenunua kwenye mitumba au kwenye maduka ya nguo.
“Ukipita kwa wauza mitumba nao utakuta wanauza nguo za jeshi, ingawa wao hufanya biashara hiyo kwa kificho, kwani huziweka sare hizo kwa nyuma ndani kwenye maghala yao na kuziuza kwa kificho na usiri mkubwa kwani wanafahamu kuwa ni kinyume cha sheria ya nchi kuuza sare hizo, ingawa wapo baadhi yao ambao huziuza hadharani wakidai kuwa ni mitumba,” ilisema.
Taarifa hiyo ilisema inawezekana kuwa kwa namna moja ama nyingine, baadhi ya watumiaji wa sare hizo, hawafahamu kuwa ni kinyume cha sheria ya nchi, kukutwa na sare yoyote ile ya kijeshi, lakini kutokujua sheria, siyo utetezi mbele ya mahakama.
Chanzo: Habari leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment