Wednesday, 9 July 2014

WANAOTUHUMIWA KUMUUA SISTA WADAIWA KUPORA BENKI




WATUHUMIWA wanaodaiwa kumuua Sista Cresencia Kapuli na kumpora Sh milioni 20, jana wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka ya wizi wa zaidi ya Sh milioni 479 katika benki ya Barclays.


Washitakiwa hao ni Hamis Shabani (34) maarufu kwa jina la Caros na Manasi Genyeka (35) maarufu kama Mjeshi, walifikishwa mahakamani hapo jana na kuunganishwa na wenzao wanaokabiliwa na kesi hiyo ya wizi.
Awali Wakili wa Serikali Mwanaisha Kombakono aliomba mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba kubadilisha hati ya mashitaka ili aweze kuwaunganisha washitakiwa hao.
Alidai kuwa washitakiwa hao na wenzao ambao walikuwa mameneja katika benki hiyo Alune Kasililika na Neema Batchu, wengine ni Kakamie Julius, Iddy Khamis, Sezary Massawe, Boniphance Muumba, Ruth Macha, Sajenti Iddy na Koplo Bundala walikula njama za kutenda kosa.
Aliendelea kudai kuwa Aprili 15 mwaka huu, washitakiwa hao wakiwa katika benki hiyo tawi la Kinondoni, Dar es Salaam waliiba fedha hizo.
Ilidaiwa kuwa kabla ya kufanya wizi huo walitumia silaha kuwatishia Anifa Ahmad na Anna Tegete ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo ili wajipatie fedha hizo bila pingamizi.
Katika mashitaka yanayowakabili askari wa Jeshi la Polisi Sajenti Iddy na Koplo Bundala wanadaiwa Aprili 16 mwaka huu katika eneo la Kijitonyama waliwasaidia washitakiwa wa wizi wa fedha hizo hizo, baada ya kitendo kutendeka.
Washitakiwa wote wanadaiwa kuiba Sh milioni 390.22 dola 55, 000 za Kimarekani na Euro 2150 mali ya Barclays.
Baada ya washitakiwa kusomewa mashitaka yao walikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Askari hao wako nje kwa dhamana ya wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh milioni 10.
Washitakiwa wengine wapo rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana. Kesi itatajwa tena Julai 22 mwaka huu

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!