Wingu jeusi limetanda katika sakata la watu wasiofahamika kupora kilogramu 15 za madini aina ya Tanzanite yenye zaidi ya thamani ya kiasi cha Sh10 bilioni katika mgodi wa Tanzanite One Mining Limited (TML), uliopo Mirerani baada ya gari maalumu lililokuwa limetengwa kupakia madini hayo kuharibika siku moja kabla ya tukio.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Douglas Swartz akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alikiri kuharibika kwa gari hilo ambalo halipenyezi risasi, lakini alidai kwamba walilazimika kutumia gari lingine aina ya Landcruiser ili kuokoa gharama za uzalishaji siku hiyo.
“Gari letu maalumu tunalolitumia kupakia madini hayo mara zote kwa bahati mbaya liliharibika siku moja kabla ya tukio na tulilihifadhi karakana, hivyo tulilazimika kutumia gari lingine,” alisema Swartz katika mahojiano maalumu na gazeti hili.
Hata hivyo, kuna taarifa kwamba tukio hilo lilipangwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya viongozi wa kampuni hiyo, wakuu wa idara ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na watu wa nje kupora madini hayo kwa lengo la kukwepa kodi serikalini madai ambayo yamepingwa vikali na Swartz.
Tukio kama hili liliwahi kujitokeza mwaka jana ambapo watu wasiofahamika walifanikiwa kupenya kimafia na kufanikiwa kuvunja chumba maalumu cha kuhifadhia madini hayo (strong room) na kisha kufanikiwa kuiba madini ya Tanzanite yenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni.
Gazeti hili limepata taarifa za uhakika kwamba kabla ya uporaji huo kufanyika juzi, madini hayo yalifungwa kwenye viroba maalumu na kisha kusindikizwa na watu watano kutoka ardhini kuelekea katika chumba cha kuyahifadhi (strong room), kabla ya waporaji kushambulia gari lililopakia madini hayo na kisha kutoweka kusikojulikana.
Vyanzo vya habari vya uhakika vilivyopo ndani ya kampuni hiyo vimeliambia gazeti hili kwamba watu hao walisindikiza madini hayo usiku bila ya kuwapo ulinzi wowote tofauti na siku zote hali ambayo imeibua maswali mengi yasiyo na majibu.
Utata mwingine ambao umejitokeza katika tukio hilo ni baada ya waporaji kufanikiwa kupenya na kuingia ndani ya kampuni hiyo, kisha kufanikiwa kufanya uporaji kirahisi ilhali ulinzi katika eneo hilo ulikuwa wa hali ya juu ukizingatia kuna uzio wa umeme, kamera za usalama kila kona sanjari na walinzi waliotanda kila baada ya hatua tano, tena wakiwa na silaha kali kama ambavyo mwandishi wa gazeti hili aliwashuhudia juzi wakati alipozuru katika eneo la tukio.
Hata hivyo, mkurugenzi wa kampuni hiyo alipoulizwa ya kwamba iweje waporaji wafanikiwe kuiba mfuko wenye kilogramu 15 wa madini hayo na kisha kuacha ule wa kilogramu 23 ndani ya gari hilo, Swartz alijibu kwa kifupi kwamba; “Huenda waporaji hawakuuona mfuko mwingine kwa kuwa ulikuwa usiku wa kiza kinene.”
Stamico
Shirika la Madini la Taifa (Stamico) lenye uwakilishi wake mgodini hapo, limetoa kauli yake na kusema kwamba hadi sasa wanahisi kuna njama zilizopangwa kwa ustadi mkubwa kupora madini hayo.
Mwakilishi wa shirika hilo ambalo linamiliki hisa kwa asilimia 50 katika mgodi huo Mhandisi, Alhonce Bikalumchi alisema kwamba pamoja na wao kuhisi hali hiyo, lakini kwa sasa hawataki kutoa kauli yoyote kwa kuwa suala hilo liko mikononi mwa vyombo vya dola
“Hata sisi kama binadamu tuna hisia kwamba huenda kuna njama ilipangwa kutokana na mazingira yenyewe, lakini hatutaki kuingia kiundani kwa kuwa suala liko mikononi mwa polisi,” alisema Bikulamchi.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba wao kama shirika wanapata hasara kutokana na kiwango cha madini hayo kuibiwa kwa kuwa wana hisa ndani ya mgodi huo na moja kwa moja lazima Serikali inapata hasara.
Juzi Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, RPC Deusdedit Nsimeki pamoja na kuthibitisha taarifa hiyo, pia alisema jeshi lake hadi sasa linawashikilia watu watano waliokuwa wakisindikiza madini ndani ya gari hilo, kutokana na kutuhumiwa kupanga njama za uporaji wa madini hayo.
Nsimeki aliliambia gazeti hili kwamba jeshi lake linawashikilia watu hao kwanza kutokana na kwamba ilikuwaje walisindikiza mzigo huo nyakati za usiku tena bila ulinzi, pili hawakukutwa na majeraha ya risasi mwilini pamoja na gari walilokuwamo kushambuliwa kwa risasi sehemu mbalimbali.
“Tunahoji kwamba haiwezekani watu wasindikize madini ghali nyakati za usiku tena bila ulinzi, pia tunawashikilia kwa kuwa pamoja na risasi kurushwa hakuna tuliyemkuta na jeraha lolote mwilini, hivyo bado tunahisi kuna njama zilipangwa,” alisema Nsimeki.
Katika hatua nyingine, mwandishi wa gazeti hili alinyang’anywa kitabu chake cha maelezo (note book) na mkurugenzi wa kampuni hiyo wakati akitoka nje kuelekea lango kuu la kuingilia kampuni hiyo, muda mfupi baada ya kumaliza mahojiano kwa sababu ambazo hazijajulikana hadi sasa na anaishikilia hadi sasa.
Pamoja na kufanya jitihada za kuomba kurudishiwa kitabu hicho, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba mara baada ya mkurugenzi huyo kuondoka nacho ndani ya gari lake huku akiwaagiza walinzi wamzuie mwandishi wa gazeti hili asisogelee katika lango kuu hilo
CHANZO-MWANANCHI
No comments:
Post a Comment