Thursday 31 July 2014

TUSIUCHEKEE UHALIFU UNAMADHARA MAKUBWA"

Ni dhahiri kwamba hali si shwati tena katika nchi yetu, kinyume na maneno au kauli nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa hata na viongozi wetu wakiwamo wa kisiasa wa kuitaja Tanzania kuwa kisiwa cha amani, utulivu na mshikamano.
Tunazo sababu nyingi za kuamini hivyo hasa kwa kuangalia idadi ya matukio ya uhalifu ambayo yanazidi kujitokeza katika miji mbalimbali nchini, hasa Dar es Salaam.
Tumeandika mara nyingi katika safu hii tukieleza jinsi ambavyo haturidhishwi hata kidogo wala kufurahishwa na ongezeko la matukio haya ya uhalifu ambayo yanazidi kujitokeza wakati mwingine mchana. Kwa bahati mbaya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama likiwamo Jeshi la Polisi, siku zote vimekuwa vikieleza mikakati yao mbalimbali ya kupambana na uhalifu.
Hatuna shaka na uwezo wao, hasa polisi ambao jukumu lao la msingi ni kulinda raia na mali zao. Tunaamini kuwa wakidhamiria uhalifu utapungua kama siyo kwisha kabisa.
Ni jambo la kusikitisha kuona kwa mfano katika jiji la Dar es Salaam, mahali ambapo hakuna shaka tunao askari wengi wa kutosha, askari wengi wa doria, miundombinu bora na kampuni nyingi za ulinzi, lakini ndilo linaloongoza kwa kuwa na matukio mengi ya uhalifu, hasa wa kutumia  silaha.
Tunakumbuka aliposhika wadhifa, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu miongoni mwa ahadi zake nyingi ilikuwa ni kupambana na uhalifu kwa akili, nguvu na utashi wake wote.
Tunachukua nafasi hii leo kumshauri IGP Mangu na timu yake nchini kote wakae kitako, wajitathmini upya, wajiangalie  kama mbinu zao za kukabiliana na uhalifu zinatosha au la wazibadili, waziboreshe na penye upungufu wauondoe.
Tunaamini kwa kufanya hivyo watakuwa wamefanikiwa kurudisha imani ya wananchi dhidi ya chombo hiki ambayo inapungua kama siyo kupotea kabisa.
Tunasema, uhalifu huu wa sasa wa kisayansi, kitaalamu unaotokea bila kificho wakati mwingine kwenye vituo kama vya mafuta, benki au kwingineko kama kwenye maduka makubwa na kusababisha vifo kama kile cha mtawa wa Kanisa Katoliki, Cresencia Kapuri miezi michache iliyopita, ni mambo yanayotisha.
Kama sehemu ya jamii, hatuna budi kukumbushana wajibu katika kujilinda dhidi ya matukio haya ya kihalifu, ingawa tunapenda polisi wetu wabadili mbinu za kiintelijensia za kukabiliana na uhalifu.
Tunaamini, wahalifu tunaishi nao mitaani, ni watoto au wajukuu zetu, wengine ni waume au wake zetu na tunaishi nao kwenye nyumba binafsi au za kupanga. Lakini ni kwa namna gani tunatoa taarifa kwenye vyombo vya dola kuhusu mienendo ya wengine ambao hairidhishi? Tunatambua nchi yetu inayo mifumo ya uongozi kama wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji. Ni kwa namna gani mamlaka hizi zinashiriki kuhakikisha watu wanaishi kwa amani, utulivu kama ilivyokuwa zamani?
Pia, tunajiuliza, ile dhana ya polisi jamii na utii wa sheria bila shurti ambayo ilianzishwa na aliyekuwa IGP, Said Mwema imefanya kazi kwa mafanikio kiasi gani katika kukabili uhalifu ambao unazidi kuongezeka katika jamii yetu?
Haya ni baadhi ya maswali ya msingi ambayo tunataka yajibiwe na kila mmoja wetu katika harakati zetu za kupambana na kutokomeza uhalifu. Tunaamini tunaweza.
MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!