Wednesday 23 July 2014

TAASISI ZA SERIKALI ZIONGEZE KASI KUPUNGUZA UMASIKINI- JK



RAIS Jakaya Kikwete ametaka taasisi za Serikali, kuongeza kasi ya kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi, akisisitiza kuwa wananchi wamekaa katika umasikini kwa muda mrefu kupita kiasi.
Amesema wanachotarajia wananchi kutoka kwa taasisi za Serikali ni kusaidiwa kutoka kwenye umasikini kwa kasi kubwa zaidi.



Alitoa maelekezo hayo juzi alipokagua shamba la kisasa la zao la buni kwenye kijiji cha Lipokela, Wilaya ya Songea, ikiwa ni moja ya shughuli zake katika ziara yake ya siku sita mkoani Ruvuma.
Rais Kikwete alisimama kwenye shamba hilo, akiwa njiani kutoka Wilaya ya Mbinga kwenda Wilaya ya Songea, ambako jana alifungua soko la kimataifa katika kijiji cha Mkenda, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
Alitoa maelekezo hayo baada ya kuambiwa kwamba pamoja na shamba hilo kubwa la buni nchini, kupata miche milioni tatu ya mibuni ya kisasa ambayo lilihitaji, lakini wakulima wa kawaida wa zao hilo la kahawa, wanashindwa kupatiwa kiasi hicho hicho cha miche.
“Kwa nini tunashindwa kupata miche milioni tatu kwa ajili ya wananchi ambayo wenyewe mmesema kuwa gharama yake ya kuizalisha ni shilingi milioni 900? Kwa nini tunashindwa kupata miche ya kutosha ili wakulima wetu wapande na kuongeza kipato chao?” alihoji Kikwete.
Alimwagiza Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Kahawa Tanzania (Tacri), Profesa James Teri kusimamia hilo.
Alisisitiza, “Hatuwezi kuwabakiza wananchi wetu katika umasikini kwa miaka mingine 30 kwa sababu tu hatuna uwezo wa kuzalisha miche ya kutosha. Hatuwezi kufanya hivyo, wameishi kiasi cha kutosha katika umasikini. “Kazi yetu ni kuwatoa watu wengi zaidi katika umasikini kwa haraka kubwa zaidi kwa sababu wamechelewa mno.
Tacri inaweza kufanya hivyo kwa kuwapa wananchi mbegu bora zaidi ya buni, ili waondokane na mibuni ya zamani ambayo uzalishaji wake uko chini. Hivyo, nataka kujua tunaweza kufanya nini kufanikisha hili siyo kuniambia habari ya changamoto ambazo TACRI inakumbana nazo katika kutimiza majukumu yake.”
Rais Kikwete alisisitiza kwamba haridhiki na kasi ya taasisi hiyo ya kujaribu kuwatoa watu katika umasikini. “Nahitaji kupata miche milioni tatu kwa ajili ya wananchi wetu. Kama iliwezekana kulipatia shamba hilo miche milioni tatu kwa nini isiwezekane kwa wananchi?”
Shamba hilo ni mali ya Kampuni ya AVIV, ambayo ni kampuni tanzu ya Kampuni ya Olam International, inayoendesha shughuli za biashara katika nchi 65 duniani.
Iliingia nchini miaka 20 iliyopita na shughuli zake kubwa ni katika mazao ya korosho na kiwanda cha kuchambua pamba kilichopo Bunda, Mara.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!