Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ameanza mkakati mpya wa kunusuru mchakato wa Katiba Mpya kwa kuitisha kikao cha wajumbe 27 wa Kamati ya Mashauriano ili kuondoa mpasuko kati ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wajumbe wengine.
Katika wajumbe hao wamo maaskofu wawili na masheikh wawili ambao Sitta amewateua kutoka katika Bunge la Katiba.
Sitta ameitisha kikao hicho jijini Dar es Salaam Julai 24 wakati kukiwa na matamko tofauti kuhusu mustakabali wa katiba hiyo, mengi yakieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyeshikilia hatima ya mchakato na wapinzani wakisema mkuu huyo wa nchi ndiye aliyesababisha suala hilo kwenda mrama.
Pia, Sitta ameitisha kikao hicho wakati viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakieleza kuwa suala la serikali mbili kwenye muundo wa Muungano, ambalo liligawanya wajumbe, ndiyo msimamo wa chama na wapinzani wakisema suala hilo halimo kwenye Rasimu ya Katiba na ndiyo sharti lao la kurejea bungeni.
Akizungumza jana katika mahojiano na gazeti hili, Sitta alisema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja kutazama mwenendo wa majadiliano katika Bunge hilo na sura 15 za katiba ili kujua yapi muhimu yanayotakiwa kupewa kipaumbele kabla ya Bunge la Katiba kuanza tena vikao vyake Agosti 5.
“Sisi tumeshapeleka barua kwa wajumbe, tumehakikisha zimekwenda na katika mkutano huo tutaelewana kuhusu masuala hayo na mengine. Wasiotaka kuhudhuria wananchi watawaelewa na wataamua iwapo nia ni kususa pekee au wenzetu wana ajenda ya siri,” alisema Sitta.
Alisema katika mkutano huo, kutakuwa na utaratibu maalumu ambao utahusisha viongozi wa dini walio ndani ya Bunge kutoka madhehebu tofauti na baadhi ya wajumbe wengine kutoka kada tofauti ndani ya Bunge hilo.
“Kutakuwa na watu karibu 27, mimi nikiwa mwenyekiti. Atakayevimba kichwa na kudharau, wananchi watajua kuwa nia yake ni tofauti na katiba,” alisema.
Sitta alisema tatizo kubwa katika Bunge hilo litakalosababishwa na kutokuwapo kwa Ukawa ni namna ya upigaji kura, lakini iwapo theluthi mbili ya wajumbe itatimia basi watakwenda kwa mwenendo huo.
“Yapo mambo muhimu zaidi katika rasimu hii kama vile tume huru ya uchaguzi, orodha ya haki za binadamu, uongozi wa asilimia 50 kwa 50 kijinsia na kuwapa Zanzibar nafasi zaidi katika Serikali ya Muungano, mambo ambayo ni makubwa kuliko muundo...ya nini kuyapiga teke yote haya na kujikita katika muundo pekee,” alihoji.
Sitta ambaye pia alipingwa kwa kumpanga Rais Kikwete kuhutubia Bunge hilo baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba tofauti na kanuni, alisema kuwa kuususia mkutano huo wa Bunge katika kipindi chote hicho siyo hasara kwa CCM, bali kwa wananchi kwa kuwa nia ni kupata katiba bora na wala siyo kukomoana.
“Iwapo Ukawa watasusia kila kitu, basi wataonyesha kuwa siyo wakomavu wa kisiasa,” alisema mbunge huyo wa Jimbo la Urambo Mashariki.
“Inashangaza kuona kuwa kila maoni yao yanaposhindwa wanasusa...iwapo watatokea watu ambao wataona Tume ya Uchaguzi haikidhi haja. Je, watatoka nje ya mkutano?” alihoji.
Kubadili sheria
Pamoja na mambo mengine, Sitta alisema upo uwezekano wa Ukawa kurudi bungeni lakini wakasusa tena kadiri mjadala utakavyoendelea. Iwapo itatokea hali hiyo, Bunge litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka theluthi mbili kufanya uamuzi.
“Katika sheria nyingine hatutakiwi kuangalia idadi. Katika mkutano wa kibiashara au Bunge la Muungano na hata Baraza la Wawakilishi, iwapo kuna wajumbe hawajatimia, basi wasiokuwapo hawahesabiwi,” alisema.
Sitta alishawahi kufanya jitihada za kujaribu kuwarudisha bungeni Ukawa siku chache baada ya kususia, lakini harakati zake ziligonga mwamba.
Lipumba atoa masharti
Wakati Sitta akifanya mkakati huo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesisitiza msimamo wa Ukawa kutorudi bungeni akisema ili warudi upande wa CCM unatakiwa kuheshimu rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba na kuepuka matumizi ya lugha chafu.
“Msimamo wetu uko wazi tu, kwamba Rasimu ya Katiba iheshimiwe. Bunge la Katiba lina kazi ya kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba, kwa hiyo lazima mjadala uongozwe hivyo, siyo vinginevyo,” alisema Profesa Lipumba.
“Kiini cha rasimu ile ni uwapo wa muundo wa Serikali ya shirikisho, yaani serikali tatu. Sasa ukienda kwenye Bunge na kuacha mapendekezo hayo na kuleta serikali mbili, unaitoa wapi?” alihoji.
Maalim Seif amvaa Kikwete
Katika hatua nyingine, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amemtupia lawama Rais Jakaya Kikwete kuwa amechangia kuukoroga mchakato wa Katiba kwa kufuata msimamo wa chama chake badala ya maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba.
Akizungumza katika kipindi cha Dk 45 kinachorushwa na ITV juzi usiku, Maalim Seif alisema kauli alizotoa Rais Kikwete wakati akilihutubia Bunge la Katiba Machi 21, mwaka huu, zimeondoa imani ya wananchi kuhusu kupatikana kwa Katiba inayotokana na maoni yao.
“Mchakato huu unamtegemea yeye. Hakuna ambaye amekamilika, Rais ajiangalie kama alivyofanya ni sawa, kama siyo sawa arekebishe mambo ili kujenga tena imani kwa wadau wote,” alisema Maalim Seif.
Alisema mwanzoni, Rais Kikwete alilichukulia suala hilo kwa busara na hekima na alipokuwa akiona mambo yanakwama alikutana na vyama na kusikiliza wanataka nini, lakini baadaye alijisahau na kusikiliza matakwa ya chama chake.
“Mfano ni hotuba yake alipokutana na Baraza la Vyama vya Siasa ilikuwa nzuri, lakini alipofungua Bunge la Katiba akajisahau kama yeye ni Rais wa Watanzania wote akachukua msimamo wa chama chake na kuihujumu Tume ya Katiba na mwenyekiti wake (Jaji Warioba).”
Katibu huyo mkuu wa CUF ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema iwapo Katiba Mpya haitapatikana wa kulaumiwa ni CCM iliyoacha ajenda kuu na kuonyesha ubaguzi wa wazi.
Alisisitiza kuwa Ukawa wanataka kijadiliwe kilichomo katika Rasimu ya Katiba na siyo rasimu ya CCM. Pia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kanuni za Bunge hilo zifuatwe.
Ushirikiano wa Ukawa
Maalim Seif alisema ushirikiano wa Ukawa utaendelea hata baada ya mchakato wa Katiba kumalizika.
“Hii ni pamoja na kuangalia kama tunaweza kuachiana majimbo ya uchaguzi iwapo chama kimoja kitaonekana kina nguvu zaidi kuliko kingine katika eneo fulani,” alisema Maalim Seif.
Alisema kama CCM ikiendelea na mchakato wa kuandika Katiba Mpya ni wazi kuwa Katiba hiyo itakataliwa na wananchi.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Maalim Seif aligusia jinsi viongozi wa juu wanavyoshirikiana katika uongozi, lakini akakiri kuwapo tatizo katika ngazi za chini, hasa kwa viongozi kutokana kutokuwa na elimu kuhusu uendeshaji wa Serikali hiyo.
Alifafanua kuwa kuna jambo ambalo hawakufanya vizuri wakati wakibadili katiba kuunda SUK kwa kutoweka kamati ambayo itakuwa inazipitia ilani za vyama vinavyounda Serikali ili kutoa ilani moja itayayotekelezwa kwa pamoja.
“Katiba yetu inasema ilani itakayofuatwa ni ile ya chama kilichopo madarakani. Hapo kidogo hatukufanya vizuri,” alisema.
Uandikishaji wapiga kura
Pia aligusia uboreshaji wa Daftari la Wapigakura na kutolea mfano Zanzibar kwamba zimekuwa zikifanyika njama ili wanachama wa CUF wasiorodheshwe katika daftari hilo.
“Ili ujiandikishe Zanzibar katika daftari, lazima uwe na kitambulisho cha ukaazi na ili upate kitambulisho hicho lazima upate idhini kutoka kwa masheha ambao hupewa maelezo na viongozi wa CCM kuwanyima vitambulisho wanachama wa CUF,” alisema.
Imeandikwa na Florence Majani, Elias Msuya na Fidelis Butahe
No comments:
Post a Comment