Friday, 18 July 2014

HISTORIA YA NYANYA ISIYOFAHAMIKA NA WENGI

Nyanya
KAMA ilivyo hulka ya binadamu wengi, si rahisi kukubali jambo au kitu kipya hata kama jambo hilo litakuwa na manufaa kwake na kwa jamii iliyomzunguka.
Karne nyingi zilizopita, mmea usiopendeza wa nyanya ulimea katika maeneo ya Andes ya Bara la  Amerika ya Kusini, lakini wenyeji wa maeneo hayo Wahindi Wekundu hawakuupanda mmea huo na hata matunda yake.
Mmea huo ulipelekwa nchini Mexico, ambako Waaziteki waliuita “Xitomati” yaani “Tomati” kubwa.


Neno tomati lilitumiwa kwa ajili ya matunda kadhaa yanayofanana na nyanya, hasa matunda yenye umajimaji mwingi.
Muda mfupi baada yam mea huo kupelekwa Maxico, Waaziteki  wakaanza kutumia matunda yake katika  mchuzi au rojo ya nyanya kwenye mapishi yao. Hatimaye pole pole mmea huo ukaanza kujulikana ulimwenguni pote.
Mwaka 1590, Kasisi wa Kikatoliki wa Shirika la Jeisut aliyeishi nchini Mexico kwa miaka mingi alilisifu tunda la nyanya na kulitaja kama tunda lenye lishe bora na virutubisho.
Jamii ya Wahispania walioishi Mexico, walituma mbegu za mmea huo nchini kwao na pia katika makoloni yao huko Ufilipino na Karrebian.
Hata hivyo, licha ya jitihada hizo zote, ilichukua zaidi ya karne tatu kabla ya nyanya kuanza kutumiwa katika mapishi uliwenguni kote.
Maoni yasiyofaa
Licha ya sifa ya nyanya nchini Maxico, tunda hilo lilichukiwa sana Ulaya. Tatizo lilianza pale wataalam wa mimea huko Ulaya walipoorodhesha nyanya katika jamii ya “Solanaceae” yaani wakiumanisha mmea huo na jamii moja ya mmea unaojulikana kama Mbeladona wenye sumu.
Mbali na mtazamo huo, wataalam wa mimea, walieleza tunda la nyanya lilikuwa na nguvu ya kuamsha  tamaa ya ngono. Watu wengine huamini  kwamba hiyo ndiyo sababu Wafaransa waliliita tunda hilo  Pomme de” Amour, yaani “Tofaa la Mapenzi”.
Maoni yasiyofaa kuhusu nyanya yalienea hadi Amerika Kaskazini, kwani mwishoni mwa miaka  ya 1820, mkulima mmoja Mmarekani kutoka Masschusetts, alikaririwa akisema kuhusu: (Nyanya): “Nilifikiri ningezila tu pindi ninapokuwa na njaa kali sana”.
Mwanaume mmoja kutoka Pennsylvania aliita nyanya kuwa ni “Takataka chungu “. Naye mkulima wa Kiingereza, alitaja tunda hilo kuwa ni “Tofaa la dhahabu linalonuka”.
Hata hivyo, katika karne ya 16  Waitaliano  waliliita tunda hilo ‘Pomodoro’, yaani “ Tofaa la Dhahabu”. Inasemekana nyanya zilipewa jina hilo kwa sababu aina za kwanza za nyanya zilizopandwa na Waitaliano  zilikuwa na rangi ya njano.
Kutopendwa hadi kupendwa
Watu walipoanza kula nyanya, mashaka waliyokuwa  nayo awali yalitoweka, na ukuzaji wa zao la nyanya ukaanza kustawi.
Hadi kufikia  miaka ya 1870, kwa kutumia  njia ya usafiri wa reli, nyanya zilisafirishwa kutoka  Calfornia na kuuzwa  New York, Marekani.
Miaka michache kabla ya wakati huo, pahala  pa kwanza pa kutengenezea Piza palifunguliwa huko Naples nchini Italia, hivyo kukawa na mahitaji makubwa ya nyanya.
Ukweli kuhusu nyanya
Kila mwaka karibia tani milioni100 za nyanya huvunwa ulimwenguni. Idadi hiyo ni kubwa zaidi ya matunda mengine makuu  ulimwenguni kama vile Matofaa, Ndizi, Zabibu na Machungwa.
Ingawa  imezoeleka nyanya ni sehemu ya kiungo katika mboga mbalimbali, kulingana na elimu ya mimea nyanya ni tunda.
Hii inatokan na  kuwa sehemu yenye mbegu ndiyo  inayoliwa (kwa kawaida sehemu  za mboga zinazoliwa ni shina, majani, na mizizi).
Kwa mujibu  wa kitabu cha The Guinness  Book  of The  Records, tunda kubwa  zaidi la nyanya kuwahi kurekodiwa lilipandwa  na  lilipovunwa  huko Oklahama, Marekani lilikuwa na uzito wa kilo 3.5.
Jambo muhimu linalopashwa kuzingatiwa katika kilimo cha nyanya ni kutokuvuta sigara karibu na mimea ya nyanya au kuishika baada ya kuvuta sigara, kwani kuna uwezekano wa mmea huo kudhurika. Sigara ina virusi ambavyo huathiri mmea wa nyanya.
Faida zinazopatikana kwenye nyanya ni nyingi. Mbali na kuwa na Vitamini A na C  , ina rangi ya asili inayoitwa lycopene ambayo huzuia kuharibiwa kwa chembe  kwa sababu ya hewa ya Oksijeni  nyingi.
Uchunguzi  uliofanywa unaonyesha chakula  kilichopikwa au rojo na mchuzi  wa nyanya nyingi  kinaweza kupunguza hatari ya kupata Kansa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!