JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemtia mbaroni mmiliki na Mkurugenzi wa Kampuni ya Lake Oil ya Mikocheni jijini humo, Ally Edha Awadhi, kwa kosa la kumtesa mfanyakazi wake kwa muda mrefu.
Taarifa zilizoifikia FikraPevu leo Julai 8, 2014 na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi katika Kanda hiyo Suleiman Kova, zinadai kuwa baada ya tukio hilo kuripotiwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay mtuhumiwa alikamatwa na kuswekwa rumande na kuwa faili la kesi hiyo limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai nchini (DCI).
Mlalamikaji anayedaiwa kupigwa na mabaunsa wa mfanyabiashara bilionea Ally Awadh wa Lake Oil
“Hilo faili halipo kwetu, lipo kwa DCI linapelelezwa na yeye kwa sasa, kwakuwa limeshatoka Kanda Maalum kwa Mpelelezi Mkuu wa Kanda na sasa huko tulishamkabidhi huyo bwana” Kova alikaririwa na FikraPevu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai nchini (DCI), Issaya Mungulu, alisema “Ngoja nitalifuatilia kuwa lipo kwa nani, inawezekana lilikuja nikiwa niko nje ya Ofisi lakini halijafika kwenye macho yangu na kama wamesema lipo kwangu ngoja nilishughulikie”
Awali Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, alinukuliwa na FikraPevu akisema “Jalada la kesi hiyo liko Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam au kama halitakuwepo kwake unaweza ukawasiliana na Kamanda wa Kanda Maalum ya Kinondoni".
Kamanda wa Kanda Maalum ya Kinondoni, Cammillus Wambura, alikiri kuwepo kwa kesi hiyo na kusema iliwahi kuripotiwa katika Ofisi yake lakini kesi hiyo ipo mikononi mwa DCI kwa ajili ya upelelezi.
Taarifa za ndani ya Jeshi hilo zilizoifikia FikraPevu zinadai kuwa, mmiliki wa Kampuni hiyo akiwa na wenzake waliohusika kumtesa mfanyakazi huyo (34-37), waliswekwa rumande wiki iliyopita na baadae kuachiwa kwa dhamana licha ya upelelezi wa kesi hiyo kuelezwa kuwa ulikuwa umekamilika.
“Walipewa dhamana na upelelezi wetu ulikuwa umekamilika na jalada lao tumelipeleka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) lakini lilirudishwa polisi kwa sababu kulikuwa na upungufu, akaagiza lifanyiwe kazi tena na sisi tulimtafuta mlalamikaji ambaye alichelewa kuja Polisi na kwa taratibu zetu ilibidi tulipeleke katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai nchini“ kilisema chanzo chetu.
Aidha, vyanzo mbalimbali vya habari vinadai kuwa mlalamikaji wa kesi hiyo aliyedai alipigwa, kudhulumiwa mali zake (yakiwemo magari) na mwajiri wake na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake, kabla hajaripoti katika Kituo cha Polisi Oysterbay Mei 2, 2013 na kisha kumwandikia barua ya malalamiko Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akidai kuwa mwenendo wa kesi yake hauendi vizuri hali iliyomfanya Waziri Mkuu kuliagiza Jeshi hilo kufanyia kazi kesi hiyo.
Mlalamikaji huyo anadai kufanyiwa unyama huo Mei 2, mwaka jana na kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni lakini akadai hakuna kilichofanywa na jeshi hilo badala yake amekuwa akipata vitisho vya mauaji jambo linalomfanya aishi kwa kujificha.
Baadhi ya mambo aliyoyalalamikia mlalamikaji ni kupigwa na kujeruhiwa, kudhalilishwa na kudhulumiwa mali zake na mwajiri wake huyo.
Alizitaja baadhi ya mali hizo kuwa ni pamoja na nyumba, magari yake mawili ambayo ni Toyota lenye namba za usajili T 786 BZG na Toyota Fortuner namba T503 BQC, bastola, fedha taslim dola za Kimarekani 100,000, maduka na ofa zake tatu za viwanja huko Kigamboni.
Katika barua aliyompelekea waziri mkuu, mlalamikaji alidai kufanyiwa unyama huo na Awadhi kwa kushirikiana na mabaunsa pamoja na baadhi ya wafanyakazi wake katika chumba maalum wakimtuhumu kuiba dola za Kimarekani milioni 10
No comments:
Post a Comment